SERIKALI imesema kwa sasa wakulima wa korosho hawatatozwa kodi kwa sababu umeundwa mfuko ambao unasimamia maendeleo ya zao hilo.
Pia imewataka wakulima ambao walipoteza mazao yao ya korosho ghalani pale ambako viongozi wao wa vyama vya ushirika watashindwa kuwalipa wawapeleke mahakamani sheria iwezi kuchukua mkondo wake.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu maswali ya hapo kwa papo kutoka kwa wabunge.
Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani ambaye alisema ingawa Serikali imeondoa tozo kadhaa katika zao la korosho, lakini imeendelea kumnyonya mkulima kwa kutoza kwa asilimia 15 ya bei ya soko.
Kwa sababu hiyo alitaka kujua mkakati wa serikali wa kumwondolea mkulima tozo hiyo ambayo ni kubwa.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema,” Serikali imefanya uamuzi wa kuondoa tozo zote. Kwenye orodha ya zile tozo ilikuwa kwenye eneo la ununuzi wa vifungashio kuna magunia na bei yake ni juu, tozo hii sasa itakuwa imeondoka kwa kuwa tumeupa mfuko unaoitwa wakfu ambao unasimamia maendeleo ya zao la korosho.
“Mfuko huu umeundwa na wadau wenyewe unachangiwa na tozo za korosho zinazouzwa nje ya nchi ambayo unachangiwa kwa asilimia 65. Na tozo hii huwa inatozwa na TRA kwa asilimia zile 65 sasa hivi mfuko huo wana fedha nyingi kukamilisha malengo ya wadau.
“Kuhakikisha masoko ya korosho yanapatikana ili kupata ubora wa korosho, tozo hii iko kwenye mfuko wa wakfu na mkulima kwa sasa hana tozo hiyo”.
Akiuliza swali jingine Katani alitaka kujua kama Serikali iko tayari kuwalipa wakulima wa korosho ambao walipoteza mazao yao ghalani.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema ni kweli uko uendelezaji wa ovyo wa vyama msingi na vyama vikuu vinavyosimamia korosho na kwamba serikali imesimamia kidete kwenye mazao yote ili kuwapo usimamizi wa dhati na wakulima wanufaike na mazao yao.