22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Wakulima Simiyu waiomba Serikali kuwasogezea Maabara ya Udongo

Na Derick Milton, Simiyu

WAKULIMA mkoani Simiyu wameiomba Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kuwasogezea huduma ya maabara ya udongo ili waweze kujua hali ya udongo katika mashamba yao pia waweze kuzalisha kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Aidha, wamesema wakulima wengi hawafahamu sifa za udongo na hali ya mashamba yao kutokana na ukosefu wa maabara hiyo hali inayosababisha kupata mavuno kidogo.

Ombi hilo limetolewa leo Jumatano Agosti 4, 2021 na wakulima hao katika Wiki ya Mkulima iliyofanyika katika mashamba darasa yaliyoko viwanja vya Nyakabindi Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Mmoja wa wakulima hao, Masiwa Bugeni amesema wakulima wengi wanapanda mazao lakini yanashindwa kustawi vizuri kutokana na kutojua hali ya udongo katika mashamba yao jambo linalochangiwa na ukosefu wa maabara ya udongo.

‘’Wakulima hatujui hali ya udongo katika mashamba yetu, pia hatujui sifa zake ndiyo maana tunapata mavuno kidogo, tunaiomba serikali itusogezee huduma ya maabara ya udongo ili tuweze kujua hali ya udongo katika mashamba yetu,’’ amesema Bugeni.

Ameongeza kuwa wamekuwa wakilima bila kuelewa mahitaji ya udongo na kwamba wakati mwingine udongo wao hauendani na mahitaji ya mbegu hali inayowakosesha mavuno licha ya kutumia mbegu za kisasa.

Naye, Enos Lupimo ameiomba serikali kuwasogezea huduma za maabara ya udongo katika mkoa wa Simiyu ili waweze kuzalisha kwa tija mazao ya chakula na biashara ikiwemo mahindi, choroko, pamba, dengu na alizeti.

Ofisa Kilimo kutoka kata ya Nyamalapa Wilaya ya Itilima, Rehema Jackson amesema wamekuwa wanawashauri wakulima wa mazao ya chakula na kilimo kutumia mbegu za kisasa pamoja na samadi ili kuboresha hali ya udongo katika mashamba yao.

Amesema changamoto ya ukosefu wa maabara ya udongo inawakabili wakulima wengi na pia wataalamu wa kilimo huwashauri kutumia samadi katika mashamba yao ili waweze kubadilisha hali ya udongo.

Kwa upande wake Isabela Mrema Mtalaamu wa kilimo kituo cha usambazaji Teknologia TARI Nyakabindi, amesema kupitia mashamba darasa wakulima wamekuwa wakipata elimu juu ya maabara ya udongo.

Amesema kuwa kupitia mashamba hayo wakulimwa wamekuwa wakielekezwa jinsi ya kuchunguza mashamba yao ambayo kwa sasa hawapati mavuno mengi.

Amesema wakulima wengi hawapati mavuno kutokana na ukosefu wa rutuba na kwamba rutuba inayohitajika kwenye udongo ina viini lishe vingi ambayo inatakiwa ichunguzwe maabara ili kujuma mahitaji ya mbolea shambani.

‘’Wakulima wengi tunawashauri watumie mbolea ya samadi, tunawashauri wawasiliane na maafisa kilimo ili sampuli za udongo wao ziweze kutumwa Ukiriguli kwa ajili ya kupimwa…’’ amesema Isabela na kuongeza.

‘’Serikali ina mpango wa kusambaza maabara za kutembea (soil kit) kupitia kwa maafisa Ugani ili waweze kutembelea mashamba ya wakulima na kuwapimia hali ya udongo katika mashamba yao’’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles