26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima Kanda ya Mashariki washauriwa kutumia vyema maonyesho ya Nanenane

Na Ashura Kazinja, Mtanzania Digital

WAKULIMA Kanda ya Mashariki wameshauriwa kutumia vyema fursa ya maonesho ya wakulima  ya Nanenane, kujifunza teknolojia mpya na ya kisasa ambayo itawasaidia kupata tija katika shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani ametoa rai hiyo mkoani Morogoro wakati akifungua maonesho ya wakulima kanda ya mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Nanenane manispaa ya Morogoro na kuhusisha washiriki kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Dk. Batilda amesema asilimia 65 ya Watanzania wamejiajiri kupitia sekta ya kilimo, ambacho kinachangia asilimia 28 ya pato la taifa, hivyo kuwataka kuongeza juhudi katika kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa ili sekta hiyo iweze kuchangia pato la taifa kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

“Tunategemea baada ya uzinduzi huu kuona wananchi wengi kutoka kwenye kanda zetu wanakuja kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika katika haya maonesho,” amesema Dk. Buriani.

Aidha, amesema kuwa maonesho hayo yana lengo la kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wadau wengine sambamba na kuongeza tija na ufanisi katika shuguli wanazozifanya.

Amesema kuwa mikoa hiyo ya Kanda ya Mashariki inakila sababu ya kufanya vizuri katika sekta ya Kilimo kutokana na uwepo wa ardhi nzuri yenye rutuba, hali ya hewa nzuri pamoja na vyanzo vingi vya maji na kwamba wakulima kufanya hivyo kutaongeza usalama wa chakula pamoja na lishe.

Sambamba na hilo, Dk. Batilda ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafugaji kufika katika maonesho hayo ili waweze kuona na kujifunza namna bora ya kupanda malisho na kuacha ufugaji wa kuhama hama ambao husababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

“Na huu ufugaji tunaozungumzia hapa sio ule wa kuhama hama, katika maonesho yetu tunawaonyesha wafugaji aina za malisho kama majani ya aina tofauti yenye virutubisho vya aina mbalimbali ili wafugaji wetu waanze kufuga kisasa, tunataka tutokane na migogoro inayotokana na ufugaji holela,”ameeleza.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Edward Gowele, amesema Maonesho hayo ya wakulima Kanda ya Mashariki kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya wakulima, wafugaji na uvuvi’, huku yakiwa na washiriki wapatao 596 na yanatarajia  kutoa elimu kwa watu zaidi ya 80,000 ambao watafika katika mabanda na vipando mbalimbali kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles