Na Denis Sikonde, Songwe
Wakulima wa zao la Pareto katika kata ya Ibaba na Itale, Halmashauri ya Ileje mkoani Songwe wameanza kunufaika na kilimo cha zao hilo, baada ya kampuni zaidi ya sita kuanza kununua kwa bei ya Sh 3,500 kwa kilo ambapo awali walikuwa wakiuza Sh 2,500 hali ambayo ilikuwa ikiwakatisha tamaa kuendeleza kilimo hicho.
Wakulima hao wamethibitisha hayo Februari 23, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ibaba kata ya Ibaba mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi baada ya mkuu huyo kutembelea baadhi ya mashamba ya wakulima akiwa na lengo la kuhamasisha kilimo hicho.
Sala Mwala ni mkulima waPPareto katika kijiji hicho ambaye amethibitisha kuwa, kilimo hicho kimeanza kuwaletea mafanikio katika kuinua pato la familia, kuliko mazao mengine ambayo walilima hapo awali, na kusisitiza kuwa pareto ni zao la uhakika ambalo kwa kipindi kifupi, wameweza kuvuna na kuuza zao hilo.
Mwala amesema kuwa, wao wanavutiwa na kilimo cha Pareto, kutokana na uhakika wa soko la kuuza, zao hilo pindi wanapovuna tofauti na mazao mengine ambayo huwalazimu kuuza kwa bei ndogo kipindi cha mavuno.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi amesema wilaya ya Ileje ni ya pekee ndani ya mkoa wa Songwe inayozalisha zao hilo kwa wingi, hivyo wananchi wanapaswa kuliweka kama zao la kimkakati kwani soko la uhakika linapatikana.
Mgomi amewapongeza wakulima hao kwa kuamua kujikita kwenye kilimo cha pareto, zao ambalo linamanufaa kwao kiuchumi lakini pia, linaendana na Tanzania ya viwanda kwa kuwa ni malighafi inayohitajika kiwandani kwa ajili ya kutengenezwa viwatilifu vya kuulia wadudu waharibifu.
“Mnatakiwa kuongeza bidii katika kilimo cha zao la Pareto kwa kuwa ni zao linalohitajika sana kwenye soko la ndani na nje, na mnatakiwa kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kujiongezea kipato sambamba na kujiinua kiuchumi,” amesema Mgomi.
Afisa Kilimo wilayani humo, Herman Njeje amesema zaidi ya tani 500 za zao hilo huvunwa kwa mwaka wilayani humo haua ambayo inatokana na mwitikio wa wataalamu wa kilimo kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima wa zao hilo mbinu bora za kutunza mashamba yao, namna ya kudumisha ubora wa zao hilo pamoja na kukabiliana na changamoto za kilimo hicho ili kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Diwani wa kata hiyo, Tata Kibona amesema kuwa kihistoria ya zao la pareto lilikuwepo miaka mingi na badaye wakulima kuacha kulima kutokana na kukosa soko, kwa sasa wakulima wameanza tena kujikita kwenye kilimo cha zao la pareto, zao ambalo linahitajika ndani na nje ya nchi, soko lake ni kubwa na liko wazi na kuongeza kuwa bado jitihada za kuhamasisha wakulima kulima zao hilo zinaendelea.