SEOUL, KOREA KUSINI
RAIA wa Korea Kaskazini waliojitenga na nchi yao wamepeleka nchini humo chupa za maji zilizojazwa mchele pamoja na bidhaa nyingine, vikiwemo vifaa vya kieletroniki.
Hiyo ni baada ya Serikali ya Korea Kusini kuzima na kuviondoa vipaza sauti katika eneo la mpakani kufuatia mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Korea hizo mbili.
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In walikubaliana wiki iliyopita kusitisha kabisa vitendo vya uhasama kuanzia jana Mei Mosi katika eneo lisilokuwa na shughuli za kijeshi.
Miongoni mwao vitendo hivyo ni pamoja na kuondoa vipaza sauti na maputo yenye vipeperushi vya kipropaganda.
Hata hivyo, aliyekuwa mfungwa wa kisiasa kutoka Korea Kaskazini, Jung Gwang-il, pamoja na wanaharakati wengine walirusha baharini chupa zilizofungwa kistadi.
Chupa hizo zilikuwa zimejazwa vitu mbali mbali ikiwemo pia dawa, pesa, na chakula kuelekea nchi hiyo, hatua ambayo haijakatazwa na Serikali ya Korea Kusini, lakini imezuiwa upande wa Korea Kaskazini.