Wakili kesi ya Dk. Tenga aomba muda

0
871

Kulwa Mzee -Dar es salaam

WAKILI wa utetezi katika kesi inayomkabili Wakili maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakugenzi wenzake, Alex Mgongolwa ameomba mahakama iwape muda wa siku tatu wazungumze na wateja wao kisha warudi mahakamani Ijumaa.

Maombi hayo yaliwalishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali, Constantine Kakula akiiwakilisha Jamhuri, alidai shauri lilikuja kwa kutajwa, lakini upande wa utetezi wana kitu wanataka kuzungumza.

“Mheshimiwa Hakimu tunaomba shauri hili liitwe Septemba 27 mwaka huu, kwa sababu ya mazingira ya kesi yenyewe, tunaomba ndani ya hizi siku tuzungumze na wateja wetu,” alidai.

Hakimu Simba alikubali maombi hayo na kuamuru shauri hilo lirudi mahakamani Septemba 27.

Ni mara ya pili kwa mawakili katika kesi hiyo kuomba muda wa kuzungumza na wateja wao. Mara ya kwanza Julai 26 mwaka huu, Wakili Braison Shayo aliomba mahakama iamuru wateja wake warudi baada ya wiki mbili atakuwa amepata muda wa kushauriana nao.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wakurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidh Shamte, Peter Noni na mshtakiwa Noel Chacha ambaye ni Ofisa Mkuu wa Fedha.

Walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Novemba 20 mwaka juzi wakishtakiwa kwa uhujumu uchumi na kutakatisha fedha zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu.

Shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote wanne na Kampuni ya Six Telecoms, ambao wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam kwa nia ya kupata fedha walidanganya kwa kutoza kiwango cha chini ya Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa mawasiliano ya simu za kimataifa.

Shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho kwa udanganyifu na kwa nia ya kukwepa malipo walishindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kama kodi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016 walishindwa kulipa ada ya uendeshaji Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Shtaka la nne linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne ambao kwa pamoja wanadaiwa walitenda kosa la kutakatisha fedha Dola za Marekani 3,282,741.12 huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la udanganyifu.

Shtaka la tano linaikabili Kampuni ya Six Telecoms ambayo inadaiwa katika kipindi hicho ilitakatisha kiasi hicho cha fedha.

Shtaka la sita linawakabili washtakiwa wote ambao wanadaiwa katika kipindi hicho walisababisha hasara ya zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu kwa TCRA.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi ulishakamilika, wanaandaa nyaraka muhimu kabla ya kuihamishia kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here