26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, November 2, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili aliyedaiwa kutekwa, hakimu washikiliwa polisi


JANETH MUSHI , ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu tisa akiwamo Wakili Pius Mbunda aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, hakimu na baadhi ya mawakili wa Serikali na watumishi wengine wanaodaiwa kula njama ikiwamo kubadili hati ya mashtaka na kumwachia huru Nelson Kangelo aliyekutwa na vipande 15 vya meno ya tembo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani keshokutwa baada ya kukamilika kwa mahojiano.

DPP alisema Kangelo alikamatwa Desemba 12, mwaka juzi na alifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na alikutwa na vipande 15 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100.

Alisema mtuhumiwa huyo alipoomba dhamana Mahakama Kuu alinyimwa na Machi 12, mwaka jana alisaini hati ya kuzuia dhamana ya mtuhumiwa huyo.

 “Aliomba dhamana Mahakama Kuu. Kwa kujua umuhimu wa maliasili zetu na kwa kujua michezo ambayo imekuwa ikijitokeza muda wote watu wanapewa dhamana wanarudi kufanya hicho walichokuwa wanafanya, na kwa kuangalia mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 36 cha uhujumu uchumi, Machi 12, mwaka jana nilisaini hati ya kuzuia hati yake ya dhamana.

 “Kutokana na zuio nililokuwa nimeliweka la kuzuia dhamana yake, Aprili 24, mwaka jana Mahakama Kuu ilimnyima dhamana na mategemeo yetu nilitegemea atakuwa rumande hadi sasa wakati upelelezi unaendelea.

“Mwishoni mwa Machi, mwaka huu, Wakili wa Serikali ambaye ni kiongozi mkuu wa mashtaka mkoani Arusha, Martenus Marandu, alinipatia taarifa kwamba amepata tetesi Kangelo yuko nje na hajui ametokaje gerezani,” alisema DPP.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo alimwagiza kufuatilia ajue ametokaje na wote walioshiriki mchezo huo wa kumtoa gerezani ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

DPP alisema baada ya Kangelo kunyimwa dhamana, Mbunda, kwa kushirikiana na hakimu anayeshikiliwa pia na Jeshi la Polisi walikula njama na wakakubaliana kupunguza thamani iliyokuwa katika hati ya mashtaka  iliyokuwa Mahakama Kuu ya Sh milioni 100 ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutoa dhamana.

 “Wakijua Mahakama Kuu imeshamnyima Kangelo dhamana, wakakubaliana wakafoji hati ya mashtaka inaonyesha thamani ya meno hayo ni chini ya shilingi milioni 10 ili Mbunda na yeye hakimu waweze kumpatia mshtakiwa dhamana.

 “Juni, mwaka jana walimpatia mshtakiwa huyo dhamana. Kama hilo halitoshi, wanajua mawakili wa Serikali si kila siku wanaenda mahakamani, wakapanga mshtakiwa atakuwa anahudhuria mahakamani Ijumaa ambayo mawakili wengine wa Serikali hawawezi kugundua na si Ijumaa tu bali ni Ijumaa mapema kabla watu wengine hawajafika na wanaahirisha kesi anaondoka.

 “Na wakapewa kiasi cha shilingi milioni  32.5 na baadaye wakakubaliana suala hilo walimalize kabisa kwa kushirikiana na watumishi wengine ndani ya taasisi nyingine ambayo majina ninayo, wakahakikisha kesi ile wanaifuta, wakamfutia mashtaka akaondoka moja kwa moja, mbaya zaidi mbali na kughushi na vitu vingine walivyofanya, wameenda wameharibu jalada la mahakama wamechoma.

“Moja ya maadili ambayo yanatuongoza ofisi ya mashtaka tunasema hatutamvumilia mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa, ni miiko na miongozo tunayoongoza taasisi hii, sitegemei kumpendelea mtu yeyote kwa kufuata cheo, kabila rangi wala jinsia na  sitegemei nifanye kazi kwa kumuonea mtu pia, miongoni mwa watu wanasema hakuna mtu mwenye zizi la wanyamapori sasa kwanini unahangaika kuwalinda, tutazilinda,” alisema DPP.

Alisema madai ya Mbunda aliyekuwa anaendesha kesi za jinai kutekwa si kweli na alikamatwa tangu Apili 28, mwaka huu na amefanikisha kukamatwa kwa washirika wenzake akiwamo mmoja aliyekamatwa juzi mkoani Kilamanjaro.

 “Wakati zoezi hilo linaendelea kuna watu wameshakamatwa, tunavyoongea kuna watu tisa wamekamatwa na wanahojiwa, jana (juzi) ilikuwa nifanye uamuzi baada ya kusoma jalada kwa baadhi ya watu ambao nimeshaona ushahidi upo, nilikuwa niwafungulie mashtaka, lakini wakati tunaenda kufungua mashtaka bado tukapata watu wengine, tumelazimika nao wakamatwe ili tupate ukweli wa kilichofanyika.

 “Nimelazimika nisimamishe zoezi hilo hadi Jumatatu, kwa sasa sitatoa majina kwa sababu za kiupelelezi, lakini kwa sababu ya jambo moja nitatoa jina la Kangelo, na  Mbunda nimelazimika kutoa jina lake kwa sababu nimeanza kuona mihemko ya watu wanajiita watetezi wa haki za binadamu, naanza kuona mihemko ya watu wanaofikiri ukishakuwa mwanasheria hauwezi kushtakiwa.

 “Nasema kama ni mhalifu bila kujali aina ya taaluma aliyonayo lazima atashtakiwa, hata kama ni mimi nimefanya kosa lazima nishtakiwe, Mbunda ni mwajiriwa wa Tanapa, ni wakili wa kujitegemea wakati Serikali tulishasema mtu ambaye ni mwajiriwa wa Serikali haruhusiwi kufanya kazi nje ya Serikali.

 “Watu wanaojiita watetezi wa haki za binadamu wakaingia mitandaoni, wakasema Mbunda amekamatwa na watu wanaosadikiwa ni polisi na kwamba walikuwa na magari yasiyo na namba zozote, lakini ukweli ni kwamba ni polisi na walikuwa na gari moja lilikuwa na namba za polisi.

“TLS imeanza kujiingiza katika mambo kama hayo kwamba wakili ametekwa na wengine akiwemo na mdogo wake anayeitwa Upendo kwamba ndugu yao  ametekwa na alikuwa anawategemea na Serikali imewaacha wakati wanajua wameenda Tanapa akawaambia inajulikana alipo, wakaambiwa wasubiri  watataarifiwa.

“Tunajiuliza kwanini wanaamua kusema taarifa za uongo kuichafua nchi, hatuwezi kufikia hatua hiyo kama ni kufanya kazi wafanye kama ni kulipa na wanaowalipa wawalipe, lakini wasichafue taswira ya nchi.

 “Mbaya zaidi wanasema kunaendelea kuongezeka na kwamba watu wanaendelea kutekwa, ukiwauliza ni watu wangapi ambao wametekwa na wametekwa lini na wapi, hawana majibu.

“Niwaombe wananchi hizo taarifa za Mbunda kutekwa zipuuzeni na yuko mikononi mwa polisi, Jumatatu na wenzake ambao tunao tutawafikisha mahakamani, aliyekamatwa Moshi naye akifungua mtandao wa wengine ambao walishiriki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles