25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wakenya wawili kizimbani

KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

RAIA wawili wa Kenya na Watanzania wawili wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kwa makosa 11 ikiwemo kula njama, kuingiza vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki bila leseni na kuisababishia Serikali na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi.

Washtakiwa ambao ni raia wa Kenya ni Beth Ngunyi (43) na Florance Dirango (34) huku Watanzania wakiwa ni Alven Swai (26) na Godluck Macha (28).

Wakili Mushi alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai Mosi na Julai 26 mwaka huu maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Washtakiwa wanadaiwa kula njama kutenda kosa la kutumia mtandao, wanadaiwa kuingiza vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki bila kuwa na leseni.

Shtaka hilo lina wakabili raia wa Kenya ambapo wanadaiwa Julai 13 mwaka huu maeneo ya Wilaya ya Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, kinyume cha sheria waliingiza vifaa hivyo vya intaneti nchini bila kuwa na leseni.

Katika shtaka la tatu washtakiwa wote wanadaiwa kusimika vifaa hivyo Julai 20 mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge Mbezi Beach na wanashtakiwa pia kwa kuvifanyia matengenezo vifaa hivyo.

Mushi anadai washtakiwa hao waliendesha vifaa hivyo, kuviunganisha na huduma ya mtandao wa intaneti na kutumia huduma hiyo ya mtandao kwa nia ya kukwepa malipo kwa kupokea na kupiga  simu za kimataifa bila kibali cha mamlaka.

Katika shtaka la tisa Beth na Florence wanadaiwa Julai 13 mwaka Kibona Lodge wakiwa sio Watanzania walikutwa nchini bila kibali.

Shtaka la 10 linamkabili Macha ambapo anadaiwa Julai 15 mwaka huu aliwahifadhi raia hao wa Kenya kinyume cha sheria.

Shtaka la mwisho linawakabili washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho walisababisha hasara ya Sh 16,634,400 kwa Serikali na TCRA.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu kesi ya uhujumu Uchumi, Jamhuri walidai Upelelezi haujakamilika na kesi iahirishwe hadi Agosti 20 mwaka huu kwa kutajwa.

Washtakiwa walirudishwa rumande hadi tarehe iliyopangwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles