31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi wa Kigogo waomba msaada wa Serikali

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Kigogo Kati, Kata ya Kigogo, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuwasaidia kupata sehemu salama ya kuishi ili waondokane na adha ya mafuriko yanayowakumba kila mwaka.

Wakazi hao ambao nyumba zao zimesombwa na mafuriko wameliambia MTANZANIA kwa nyakati tofauti kuwa hawajakataa kuhama kama agizo la Serikali lilivyotolewa lakini hawajui watakapohamia.

Mmoja wa wakazi hao, Msimbe Gunewe alisema hata akihama katika eneo hilo hatarishi anafamilia ambayo hajui atakapoipeleka.

“Hatujakataa agizo la Mkuu wa Mkoa(Paul Makonda) na Serikali kwa jumla bali hatuna mahali pa kuhamia wala usafiri wa kututoa hapa, nina familia ya watu nane nitahama vipi,?” alihoji Gunewe.

Alisema anaiomba serikali kuwapatia viwanja na kuwawezesha fedha za kujengea ili waweze kuondoka katika eneo hilo.

Naye Maua Nassoro, alisema changamoto ya mafuriko si ya mwaka huu tu kwa kuwa mto huo umesomba nyumba nyingi zilizokuwa nyuma ya nyumba yake na sasa yeye amefikiwa.

“Sina jinsi ya kufanya maana vyumba vitatu vimeondoka na maji wapangaji wamenikimbia na nina familia sina pa kuipeleka,” alisema Maua.

Aliongeza kuwa Serikali iangalie tatizo hilo kwa kuwa awali hawakuwa katika hatari hiyo.

“Tatizo ni kona ya mto ambayo ilirekebishwa baada ya kuonekana mto unakwenda katika makazi ya watu hivyo walileta kijiko na kutoboa njia nyingine ya maji,” alisema Maua.

Kwa upande wake, mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Ramadhani Ally alisema chanzo cha kubomoka kwa nyumba hizo ni urekebishaji wa mto baada ya watu kujenga maghala na kubana njia yake.

“Kuna kipindi mto huu ulikosa mwelekeo na kufuata makazi ya watu wengi, ndipo mbunge wa kipindi hicho, Idd Azzan alipoleta kijiko kurekebisha,” alisema Ally.

Alisema badala ya kuurudisha mto katika eneo lake ukaelekezwa eneo hilo na kusababisha kuanza kusomba nyumba zilizopo.

“Ni nyumba nyingi zimesombwa na mto unazidi kusogea huku na kuacha kule kwenye mashamba ulikokuwa awali hivyo tunaiomba Serikali itusaidie kuleta kijiko na kuuhamisha kurudisha ulikokuwa,” alisema Ally.

Nyumba na nne za mtaa huo zimebolewa na mafuriko yaliyotokea baada ya mvua zilizonyesha juzi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles