22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi Liwiti watakiwa kufanya usafi bila kushurutishwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Liwiti, Ignas Maembe, amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi bila kushurutishwa na kulipa ada za uzoaji taka kwa wakati.

Akizungumza na wananchi wakati wa usafi wa mwisho wa mwezi amesema ni jukumu la kila mmoja kuzingatia suala la usafi wa mazingira ili maeneo yote yawe safi.

“Tumewahamasisha wananchi wamejitokeza na kufanya usafi katika maeneo yao, lengo ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kujenga tabia ya kufanya usafi bila kushurutishwa. Usafi wa mwisho wa mwezi ni mwendelezo wa kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa safi,” amesema Maembe.

Mtendaji huyo pia amewataka wananachi kulipa ada za taka kwa wakati ili kumrahishia kazi mkandarasi na kuepuka taka kurundikana.

“Kila mwenye nyumba hivi sasa anao waraka ambao unamuelekeza vitu gani anatakiwa kufanya likiwemo suala zima la usafi wa mazingira kwahiyo hatutarajii tukute eneo la mtu chafu,” amesema.

Naye Ofisa Afya Kata ya Liwiti, Thuwaiba Abdallah, amesema wamekuwa wakishirikiana na kamati za mazingira na polisi jamii kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira.

“Kuna changamoto ya utiririshaji maji machafu na utupaji taka ovyo kwenye mifereji, nawashauri wananchi usafi iwe ni tabia usiishie tu Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Unapofanya usafi unajiepusha na magonjwa ya maambukizi, mazalia ya mbu yote yataondoka na magonjwa yatapungua,” amesema Thuwaiba.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Amina Kijazi, amesema wananchi wamekuwa na mwamko wa kufanya usafi katika mazingira yao.

“Tulipita kila nyumba tukiwahamasisha wananchi na wengi wameitikia na wametoa takataka, pia tunashukuru manispaa wametuletea gari kubwa la kubeba taka…tuweke mazingira yetu safi si lazima tusimamiwe,” amesema Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles