32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wakandarasi wazembe Mwanza kikaangoni, wategwa miradi mipya

Na Clara Matimo, Mwanza

Wakandarasi wazembe wasiomaliza miradi kwa wakati katika Mkoa wa Mwanza wameonywa kuwa hawatavumiliwa na hawatapewa miradi mipya ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Afisa Mchunguzi Mkuu kutoka ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Maua Ally(aliyesimama) akiwapa elimu wahandisi wa mkoa huo iliyolenga kuwakumbusha  maadili katika utekelezaji na usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa Septemba 29, 2022 na Katibu Tawala Msaidizi, Seksheni ya Miundombinu Mkoa wa Mwanza, Mbunifu wa Majengo, Chagu Ng’homa wakati akizungumza na wataalamu wa ujenzi pamoja na mameneja wa  Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kutoka wilaya zote saba zilizopo mkoani humo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Balandya Elikana.

Ng’homa amesema hata ambao walipewa kazi na hawajamaliza wajipange maana watawaondoa kwani hawawezi kuendelea kusimamia wakandarasi ambao hawana uwezo pia amewataka watakaopewa miradi waitekeleze kwa viwango kulingana na mikataba yao.

“Kwa kuwa mkoa umepewa mamlaka ya kusimamia miradi ya maendeleo ndani ya mkoa  hivyo  mkandarasi ambaye hataweza kukidhi mahitaji ya mkoa kwa kweli hatutamtaka tena kwa miradi hii ya mwaka wa fedha 2022/2023,”amesema  Ng’homa.

Aidha amewataka watumishi wa umma ambao wamepewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo kujiepusha na vitendo vya rushwa kutoka kwa wakandarasi ili miradi inayotekelezwa iendane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na serikali.

“Ili miradi ya maendeleo itekelezwe kwa tija lazima uwajibikaji, uadilifu na weledi  uwepo kwa watumishi  na wataalamu wa umma tuliopewa dhamana ya kuisimamia sasa ukiweka masuala ya rushwa mbele inamaana kuna miradi ambayo itakwama kutekelezwa kwa ubora.

“Nitoe mfano mtumishi umechukua asilimia kumi ya utekelezaji wa mradi inamaana yule anayetekeleza huo mradi kama ni mkandarasi au fundi atapigia hesabu ya hiyo asilimia kumi kwa hiyo kazi ambayo ingeweza kufanyika  kwa asilimia kumi uliyoichukua haitafanyika mwisho wa siku ule mradi unakuwa chini ya kiwango,”amesema.

Akizungumzia hali  ya utekelezaji wa miradi mkoani Mwanza mbunifu huyo wa majengo amesema: ”Tunajivunia mkoa wetu maana miradi mingi imeenda vizuri na leo tumekuja kuwekeana mikakati ya kuendelea kuboresha zaidi miradi yetu kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023  ili tufanikishe haya ni lazima tuwe na weledi kwenye Utekelezaji wa miradi,”amesema Ng’homa.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Goodluck Mbanga amesema bajeti ya kutekeleza miradi ya barabara Mkoani humo imekua ikiongezeka kila mwaka huku akibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha  2022/23 imetengwa zaidi ya Shilingi Bilioni 25 na  kuna mikataba zaidi ya 90 itatekelezwa tofauti na 2021/2022 ilipotekelezwa mikataba 43.

“Mwaka 2021 Tarura mkoa wa Mwanza tulikuwa na bajeti ya Sh bilioni 11 mwaka jana 2022 ilipanda hadi bilioni 24 na mwaka huu tunaongelea bilioni 25 kwa upande wa mikataba mwaka 2021 tulikuna na mikataba 43 saizi tunamikataba zaidi ya 90 hii imetokana na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza fedha katika miundombinu ya barabara,”amesema Mhandisi Mbanga.

Washiriki wa kikao hicho walipewa elimu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza iliyolenga kuwakumbusha  maadili katika utekelezaji na usimamizi wa fedha  za miradi ya maendeleo ikiwemo  miundombinu ya barabara.

Akitoa mada ya Maadili na Changamoto za Rushwa kwenye utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Afisa Mchunguzi Mkuu kutoka ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Maua Ally aliyemwakilisha Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo mkoani humo, Elisante Mashauri amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa hasa katika kuwapa kazi wakandarasi  wasio na sifa kwani ina madhara mengi kwa taifa ikiwemo kutekelezwa kwa miradi isiyo na ubora uliokusudiwa.

 “Rushwa inamianya mingi kwenu wahandisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia kwenye mchakato wa zabuni ambapo wanaopenda rushwa huvujisha siri za zabuni kwa wanaoomba kazi hivyo inasababisha kuwapa kazi wakandarasi wasio na sifa hali hiyo inafanya kushindwa kusimamia taaluma yenu pamoja na mikataba.

“ Inasababisha muandae taarifa za uongo na mwisho mnashindwa kuwachukulia hatua stahiki wakandarasi waliokiuka mikataba hivyo nawasihi kuweni wazalendo na waadilifu katika kutekeleza majukumu yenu msijihusishe na rushwa   maana rushwa siyo dili haina manufaa yoyote bali ni dhuluma na dhambi hata kwa Mwenyezi Mungu”amesema Maua.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi, Seksheni ya Miundombinu Mkoa wa Mwanza, Mbunifu wa Majengo, Chagu Ng’homa lengo la kikao hicho ni kufanya tahmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopita ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kuona changamoto zilizojitokeza ili kuweka mikakati ya kuzitatua kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi ya mwaka 2022/2023.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles