25.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

Wakandarasi watakiwa kutekeleza miradi kwa wakati ili kulinda uaminifu

Na Clara Matimo, Ukerewe

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022, Sahili Geraruma, amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umma nchini kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati ili waendelee kuaminiwa na Serikali.

Geraruma ametoa agizo hilo  leo Julai 16, 2022 akiwa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza    baada ya kupokea taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Halmashauri–Airport inayojengwa Mjini Nansio kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.0 na upana mita 8.5 kutoka kwa Menjeja waWakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Leonidas Sospeter ambaye amesema Mkandarasi anayeutekeleza ameomba aongezewe muda wa siku 30.

Mhandisi Sospeter amesema ujenzi wa mradi huo uliibuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili kuwezesha barabara hiyo kupitika muda wote ulianza Januari 5, 2022 ulitakiwa kukamilika Julai 4, mwaka huu lakini kutokana na changamoto za mvua zilizokuwa zinanyesha Mkandarasi anayeutekeleza ambaye ni Intercountry Contractor aliomba aongezewe muda. 

“Ujenzi wa barabara hii ambayo inasimamiwa na ofisi ya Meneja wa Wilaya Tarura wilayani hapa unatekelezwa kwa fedha za miradi ya Maendeleo kutoka Mfuko wa Barabara za mwaka wa fedha 2021/2022  fedha iliyoidhinishwa ni Sh 500,000,000.00, Mkandarasi alisaini Mkataba wa Sh 493, 498,000.00 hadi sasa fedha iliyokwishapokelewa ni Sh 500,000,000.00 sawa na asilimia 100, Mkandarasi ameishalipwa Sh 267,868,000.00 sawa na asilimia 54.27 ya fedha iliyosainiwa kwenye mkataba wa malipo.

Baada ya maelezo hayo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2022, Geraruma kabla hajaweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo, akasema ingawa wakandarasi wanaruhusiwa kisheria kuomba muda wa nyongeza kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wanatekeleza miradi lakini wanapoomba kuongezewa muda wanapunguza kiwango cha kuaminiwa na wateja wao pia wanachelewesha nia ya serikali kuwapa wananchi wake huduma mapema.

“Wakati mnaomba tenda za kutekeleza miradi mhakikishe mnaweka muda ambao mna uhakika hata kama mtakutana na changamoto lakini mtakamilisha kwa wakati ambao mmeusema nyie wenyewe extension siyo nzuri sana japo inaruhusiwa kisheria,”amesema Geraruma.

Awali, akizungumza  baada ya kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, katika Kijiji cha Bukimwi Kata ya Ngoma, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Kanali Denis Mwila, amesema utakimbizwa Kilomita 102 ambapo  utazindua,utaweka jiwe la msingi na kukagua miradi sita yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 1.17.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ukerewe(CCM) Joseph Mkundi, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo jimboni humo ambapo aliwasihi wananchi kuitunza ili waweze kuitumia kwa muda mrefu.

Mwenge huo unaoongozwa na Kauli mbiu isemayo ‘Sensa ni Msingi wa Mpango wa Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Malengo ya Taifa’utaondoka Wilayani Ukerewe kesho alfajiri Julai 17 kuelekea Halmashauri ya jiji la Mwanza ambapo miradi yote iliyokaguliwa, kuwekewe mawe ya msingi na kuzinduliwa imetekelezwa kwa kiwango ikiwemo ya afya, elimu na barabara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles