26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Wakandarasi Muleba wapewa onyo

Na Nyemo Malecela, Kagera

WAKANDARASI wanaojenga barabara ya wilayani Muleba, mkoani Kagera wametakiwa kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kama ilivyokusudiwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila wakati alipotembelea na kukagua miradi ya barabara inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) mwaka wa fedha 2020/2021.

Katika ziara hiyo, Nguvila alitembelea barabara ya Posta-Bomani iliyojengwa kwa kiwango cha lami iliyogharimu sh. 333,689,120 barabara za Tukutuku-Kaigara na Fatuma-Buyango zilizofanyiwa matengenezo ya kawaida zilizogharimu sh. 122,330,000 na mtaro wa Buhimba uliopo barabara ya Blasio Kaganda uliogharimu sh. 68,962,000 wenye urefu wa mita 771.

Amewataka wakandarasi wote wanaopewa kazi katika wilaya hiyo kuhakikisha wanazitekeleza kwa umakini, uzalendo na viwango vinavyostahili ili miradi hiyo idumu.

Nguvila amewataka wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa viwango na wahandisi kuongeza umakini katika usimamizi ili miradi hiyo iweze kudumu kwa manufaa ya wananchi.

“Serikali inatoa fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye jamii lakini wanaopewa jukumu la kutekeleza miradi hiyo wanakuwa si wazalendo kwa kuangalia maslahi yao matokeo yake miradi inatekelezwa chini ya viwango na haidumu.

Binafsi nitakuwa mkali kwa wakandarasi wote mtakaopewa kazi na kushindwa kuitekeleza katika viwango bora,” ameeleza Nguvila.

Nguvila amewataka wakandarasi kuhakikisha wanatengeneza vivuko kulingana na uhitaji wa makazi ya wananchi na kufanya marekebisho yaliyobainishwa wakati wa ukaguzi kabla ya muda wa matazamio kuisha.

Pia amewaagiza  Tarura  kuwasiliana na Wakala wa Barabara (TANROAD) kuweka kalavati kwenye barabara ya Fatuma-Buyango ambayo imepakana na barabara kuu ili kuzuia maji kuingia eneo la barabara kuu, ikiwa ni pamoja na kuzibua mitaro.

Nao wakazi wa eneo la Buhimba kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa ujenzi wa mtaro wa kupeleka maji bondeni barabara ya Blasio Kaganda ambayo yalikuwa kero na kusababisha hatari kwa makazi yao umesaidia kuwaondolea adha waliyokuwa wakiipata kipindi cha mvua na kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa mtaro huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles