NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umewataka Watanzania kuzingatia Sheria ya Misitu Namba 14 ya Mwaka 2002, Kanuni za Misitu za Mwaka 2004 na Mwongozo wa Uvunaji Endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu nchini wa Mwaka 2015, kuhusu uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao ya misitu hususani mkaa ili kuepuka adhabu.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali za Misitu na Nyuki wa TFS, Mohamed Kilongo, amesema sheria iliyopo pia imezuia usafirishaji wa mazao yote ya misitu ikiwamo mkaa nyakati za usiku.
Aidha, alisema Serikali inawataka wasafirishaji wote wa mazao ya misitu pamoja na mkaa watumie usafiri wa magari yenye magurudumu manne pamoja na kuzingatia sheria ya kulipa ushuru wa Sh16,600 kwa kila gunia moja lenye ujazo wa kilogramu 75.
“Kilo moja ya mkaa inatakiwa ilipiwe Sh 240 na hatutaki mkaa uwe biashara tunachotaka ni mkaa ubaki kwa matumizi ya kawaida majumbani,” alisema Kilongo.
Alisema udhibiti wa uuzaji mkaa kiholela utasaidia kupunguza ukataji miti ovyo ambao ulikuwa umeenea katika maeneo mengi ya hapa nchini.
Kilongo alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya wananchi kujenga mazoea ya kukata miti ovyo bila kupanda mingine hali ambayo ni hatari kwa baadaye.
Amewashauri wananchi kuzingatia sheria ili kulinda misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.