Na Clara Matimo- Mwanza
Wajumbe watatu wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe na Mkoa wa Mwanza wameapishwa leo Machi 15 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ofisini kwake huku akiwataka kufanya kazi kwa weledi kuepuka vishawishi vya rushwa, kwani kuna watu ambao watajaribu kuwarubuni ili kupindisha haki.
Pia ametoa rai kwa halmashauri zote za mkoa huo kuhuisha mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji yaliyomaliza muda wake na kutoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza hayo ili wajue majukumu yao pamoja na kuendelea kutenge bajeti kwa ajili ya kuwawezesha washauri kupata vitendea kazi ikiwemo shajara na usafiri.
“Wajumbe mlio kula kiapo leo fanyeni kazi kwa weledi kuepuka vishawishi vya rushwa mtaingia kwenye migogoro ambayo wenye fedha wanataka kuwadhulumu wanyonge wasio na fedha mjue hilo lipo katika masuala ya kutafuta haki ninyi msimamie haki, mumtangulize Mungu kwenye kufanya maamuzi yenu na mfuate kanuni, taratibu na sheria ili kujenga imani kwa jamii mkawe faraja kwao na siyo kukuza migogoro na kuchelewesha upatikanaji wa haki,”amesema na kuongeza
“Tambueni kwamba kutokana na ongezeko la migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi katika mkoa huu serikali iliona upo umuhimu wa kuanzisha mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya katika wilaya za Mwanza, Ukerewe na Sengerema na hivyo kuwa na jumla ya mabaraza matatu katika mkoa wetu lengo ni kuhakikisha migogoro hiyo inatatuliwa, jamii itakiheshimu chombo chenu endapo ninyi mtatenda haki,”alisisitiza Mhandisi Gabriel.
Aidha amewataka watumishi wa mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya waendelee kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na itakayokuwa inatolewa ili kuboresha utoaji wa huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi na kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu shauri kufunguliwa katika baraza maana wajibu wa mkoa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za ardhi zinatolewa kwa weledi na uadilifu.
“Lakini kama mkisikiliza vizuri kwa kuzingatia weledi mkapata ukweli yawezekana mkatumia muda mfupi zaidi ili kuondoa changamo hiyo maana idadi ya migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi imeendelea kuongezeka siku hadi siku,”amesema mkuu huyo wa mkoa.
Pia amewaasa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kutumia huduma za mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ambayo washauri wake wameapishwa leo ili waweze kupata ufumbuzi wa migogoro yao kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wao wajumbe walioapishwa ambao ni Blandina Limihagati wa baraza la ardhi na nyumba Wilaya na Mkoa wa Mwanza, Sijo Maira na Muyengi Munubi wa baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Ukerewe wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki ili kutokumuangusha Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Angeline Mabula kwa kuwateuwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari baada ya kula kiapo wajumbe hao wamesema hawatampendelea mtu yeyote katika kutoa maamuzi watatekeleza majukumu yao kwa uaminifu , uadilifu na utiifu pia kwa kusimamia sheria.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe, Kato Conrad, amesema wajumbe hao watawasaidia kusikiliza migogoro ya wananchi itokanayo na matumizi ya ardhi na kuamua mashauri yao kwa wakati kama kanuni zinavyowaelekeza hasa ikizingatiwa kwamba wao ni wenyeji wa maeneo ambayo yanabishaniwa mbele ya baraza hata kama masuala ya mila na tamaduni yakiibuka mahakamani.
Mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ni miongozi mwa vyombo vilivyoundwa chini ya kifungu cha 167 cha sheria ya ardhi sura ya 113 kwa ajili ya kusikiliza na kuamua migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi nchini uanzishwaji wa mabaraza hayo unazingatia sheria ya mahakama za ardhi sura ya 216 kifungu cha 22(1).