CHRISTINA GAULUHANGA
Zaidi ya wajumbe 200 wanatarajiwa kushiriki mkutano wa kimataifa wa Shirikisho la Taasisi zinazotoa Huduma za Anga na Kuongoza Ndege (CANSO), kwa kanda ya Afrika utakaofanyika nchini wiki ijayo ambapo watajadili teknolojia ya kisasa pamoja na uongozaji ndege.
Akizungumza leo Agosti 29, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Hamza Johari ambaye pia ni Mwenyekiti wa CANSO wa Kanda ya Afrika amesema katika mkutano huo mada mbalimbali zitachambuliwa na kutoa suluhu jinsi ya kuondoa vikwazo katika Sekta hiyo pamoja na kuwa na mifumo ya uongozaji ndege inayofanana.
Amesema katika mkutano huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele atakuwa mgeni rasmi ambapo mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ya ‘Kuelekea Anga isiyo na mipaka barani Afrika na mchango wake katika kizazi kijacho cha wataalam wa usafiri wa Anga.
Aidha ameongeza kuwa wajumbe watajadili ni jinsi gani nchi wanachama wa Kanda ya Afrika wataboresha ushirikiano na kujadili changamoto ya kuepusha uwezekano wa ajali katika ndege zisizo na rubani (drons).