25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Wajue ‘wanawake twiga’ wa Burma

duu

NA JOSEPH HIZA,

WANAWAKE wa kabila la Kayan katika Jimbo la Kayah lililopo Mashariki mwa nchi ya Burma, ambayo pia inajulikana kama Myanmar hunyoosha shingo zao kwa pete za shaba nyeupe kwa kile wanachoona ni alama ya urembo kwa utamaduni wa Kayan.

Kwa sababu hiyo, wanawake hao kwa utani hujulikana kama wanawake twiga.

Kabila hilo pia hujulikana kama Padaung, na 50,000 wanaishi katika misitu minene magharibi mwa Mto Salween na maeneo kuzunguka vilima Pekon, katika jimbo hilo, pia jimbo la kusini la Shan Mashariki mwa Myanmar.

Mji wao wa asili ni Loikaw uliopo kaskazini magharibi mwa nchi na leo hii wanaishi zaidi katika vijiji saba vilivyokizunguka kijiji chao kikubwa cha Bangpe.

Wengine 500 wanaishi nchini Thailand katika vijiji vitatu vilivyopo ndani ya Wilaya ya Muang, Jimbo la Mae Hong Son, karibu na mpaka wa Myanmar.

Kabila hilo mara ya kwanza liliwasili Thailand mwaka 1988 wakati walipokimbia mapigano baina ya askari wa Burma na makabila ya walio wachache katika Jimbo la Kayah.

Kwa lugha yao wenyewe, Padaung hujiita Kakaung, ikimaanisha watu wanaoishi katika vilele vya vilima.

Lugha ya Padaung kwa karibu inahusiana na ile ya kabila la Lahta nchini Myanmar na ni sehemu ya tawi la Karen la familia ya Tibeto-Burman.

Tukirudi na uvaaji wa koili au mzingo wa shaba shingoni, huzifanya shingo za wanawake kuonekana ndefu, ijapokuwa kiuhalisia uzito wa pete huishusha misuli eneo la mtulinga na kugandamiza kizimba cha mbavu zinaonekana kuwa ndefu kuliko zilivyo.

Kwa sababu hiyo, kinyume na imani iliyoenea, koili hizo hazirefushi shingo na hivyo zinaweza kuondolewa bila shingo kupinda au kuhisi maumivu na baada ya wiki kadhaa hurejea katika hali ya kawaida.

Wakati wanawake wa kabila hilo wakibakia nyumbani, wanaume huenda kuwinda msituni na wakati mwingine wanyama wa mwituni huja kijijini na kushambulia watu.

Simulizi za kale zinadai kwamba koili hizo shingoni ziliwalinda wanakijiji dhidi ya mashambulizi ya wanyama wakali kama tiger, kwa vile jamii hiyo ya paka huwashambulia walengwa wake shingoni.

Nadharia nyingine inadai koili ziliwasaidia kuwazuia wanaume kutoka makabila mengine hasimu kuwatamani wanawake wao.

Nadharia nyingine zinadai zililenga kuwatofautisha wanawake wa kabila hilo na wengine wa makabila madogo madogo.

Siku hizi hakuna mtu anayekumbuka sababu halisi iliyosababisha uvaaji wa pete shingoni lakini watu bado wanafuata utamaduni huo katika baadhi ya vijiji.

Inastaajabisha kuona hivyo kwa sababu ni nadra kwa kabila kuendelea kushikilia utamaduni wao. Sehemu nyingi zimechanganyika na tamaduni mpya na za kisasa lakini si wanawake wa Kayan.

Leo hii, watu wanaamini kinyume, kwamba urefu wa shingo zao ndio huwafanya wanawake kuwa warembo zaidi—na imefikia kwa wanawake hao kuvaa pete za dhahabu kama nyongeza ya urembo.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, baadhi ya wanawake wanafurahia kuendeleza utamaduni huu lakini wengine wanahisi kushinikizwa kuuendeleza hasa nchini Thailand, ambako umelenga maslahi ya kiuchumi.

Miongo miwili iliyopita wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya waasi wanaotaka kujitenga wa Karenni na jeshi la Burma kama tulivyoona awali ulisababisha baadhi ya wakazi wa Kayar kuikimbia Myanmar.

Thailand iliwapatia wakimbizi hao wa Kayan makazi ya muda chini ya hadhi tata ya ukimbizi ambayo ilishuhudia watu zaidi ya 500 wakiishi katika vijiji vinavyolindwa kaskazini mwa mpaka wa Thailand.

Hivyo, utamaduni wao wa kipekee ulizua wazo la kuundwa kwa vijiji vya utalii mwaka 1985, wanawake wakilazimishwa kuishi kwa utalii. Lakini bila uraia, watu hao wa Kayan wana ukomo wa kupata stahili za huduma za umeme, afya na elimu.

Zaidi ya hayo mamlaka za Thai zilikataa kuwaruhusu Wakayan kukaa nje ya vijiji vya kitalii zikidai wao ni wahamiaji wa kiuchumi na si wakimbizi halisi.

Watalii wanaokadiriwa kufikia 40,000 kila mwaka hulipa ada ya dola nane na 16 za Marekani kutua katika vijiji hivyo vilivyopo milimani linakoishi kabila hilo waweze kujionea na ‘kushangaa’ mwonekano usio wa kawaida na kupiga nao picha.

Bahati mbaya ni kwa nadra ada inayoingia kusambazwa moja kwa moja kwa wanakijiji. Badala yake wanawake wanaovalia pete shingoni huuza vitu vingine wanavyobuni kwa mikono yao katika maduka ya kitalii ya bidhaa za mikono.

Wakazi wengine wa ujumla wao hushindia posho ya chakula na faida iliyotokana na mauzo ya bidhaa za mikono huku wanawake twiga wakipewa mshahara wa ziada.

Wamiliki wa vijiji hivyo nchini Thailand hupunguza mishahara iwapo wanawake watafumwa wakiwa na wageni wakiwasilimulia masaibu yanayowakumba au kukutwa wakitumia vitu vya kisasa kama vile simu za mikononi au kompyuta.

Wakati wengine wakidai vijiji hivyo huwapa Kayan fursa ya kuendeleza utamaduni wao, wakosoaji wanalaani utaratibu huo kuwa unawanyonya wanawake na watoto hawa wasio na utaifa kwa kujipatia dola za watalii kwa mgongo wao masikini hao.

Ijapokuwa maadili ya mpangilio huu huwafanya baadhi ya wasafiri kujisikia vibaya, magari yaliyojaza wageni wenye shauku bado hutembelea vijiji hivi.

Kampuni nyingi za kigeni hujaribu kuendesha kampeni ili kuzisitisha kupinga kile wanachokiona unyonyaji wa wamiliki wa vijiji dhidi ya kabila hilo, zile zilizopo Thailand huzipigia chapuo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles