TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM
JUMUIYA ya watu wenye Ulemavu ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), wameanza kuchangisha fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu ya kugombea urais, Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.
Akizungumza wakati wa mkutano wao uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mwenyetiki wa Jumuiya hiyo, Peter Sarungi alisema wamefurahishwa na utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli hasa kwa kuwajali watu wenye ulemavu.
Alisema ilani ya sasa imebadilisha maisha ya walemavu kwa kuwa imetekelezwa kwa asilimia 99.
“Awamu hii imeweza kuwashirikisha vema walemavu kwa kuwateua viongozi wenye ulemavu na kuunda wizara inayoshughulikia walemavu, haijawahi kutokea,” alisema Sarungi.
Alisema sababu nyingine ya kumchukulia fomu, ni kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa kuwapa mikopo kupitia halmashauri nchi nzima ambapo wengi wamenufaika.
“Kwa Manispaa ya Ilala pekee, zaidi ya bajaji 2,000 ndani ya mwaka 2018/19.
“Pongezi kwa Mkurugenzi wa Ilala (Jumanne Shauri) kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 1.3. kukuza na kuwesha michezo ya walemavu katika ngazi za kimataifa ambapo timu ya Tembo Warriors kwenda Angola,” alisema Sarungi.
Alishauri chama hicho kuendelea kuwawezesha walemavu kushiriki masuala ya kiuchumi kwa kuweka sera wezeshi zitakazowawezesha kushindana na wasio na ulemavu katika ilani.
“Tunaomba Serikali kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kutoa ruzuku kugharamia elimu kwa walemavu wanaochaguliwa vyuo badala ya mikopo ilivyo sasa,” alisema Sarungi.
Alisema wanaomba kuanzishwa kwa mipango maalumu wa bima za afya kwa walemavu kutoka kwa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma hizo kama ilivyokuwa kwa wazee na watoto.
Baadhi ya watu wenye ulemavu wameziomba manispaa nyingine za jiji hilo kuiga mfano wa manispaa ya Ilala kwa kutoa asilimia mbili ya mapato yake kuwakopesha watu wenye ulemavu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MTANZANIA, baada ya mkutano walisema halmashauri zingine zinachelewesha kutoa mikopo hiyo na kusababisha watu wenye ulemavu kukimbilia katika manispaa ya Ilala.
Mmoja wao, Said Mwigombi alisema alipeleka maombi ya kupata mkopo Manispaa ya Temeke, lakini kutokana na kuchelewa alilazimika kujiunga na wenzke Ilala.
Katibu wa Jumuiya hiyo, John Labu alisema wanatoa shukrani kwa serikali kutekeleza ilani ya CCM kwa kuwajali watu wenye ulemavu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel alisema haijawahi kutokea tangu uhuru mambo ya walemavu yakabebwa na kutekelezwa vema kama yanavyotekelezwa sasa.