22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Wajawazito wasisitizwa kutumia vyakula vya asili

Na YOHANA PAUL – MWANZA

WAJAWAZITO wamesisitizwa kuwekea mkazo suala la ulaji wa vyakula vya asili, zikiwemo mboga mboga na matunda kwa wingi ili kuepuka tatizo la upungufu wa damu kipindi chote cha ujauzito.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Ofisa Mhamasishaji Mpango wa Damu Salama Kanda ya Ziwa, Benardinho Ivomedaa alipozungumuza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani Mkoa wa Mwanza.

Ivomedaa alisema wajawazito ni miongoni mwa kundi lenye uhitaji mkubwa wa damu kutokana na wengi wao kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, hivyo ni lazima wachukue tahadhari mapema kwa kula vyakula vyenye madini ya chuma kwa wingi ambavyo husaidia kuongeza damu mwilini.

Alisema kwa siku za hivi karibuni ipo changamoto kubwa kwa wajawazito wengi kupungukiwa damu wanapojifungua kwa sababu ya mfumo wa maisha ya kisasa kwa wengi wao kutumia muda mwingi kwenye mitandao na kusahau kufanya mazoezi pamoja na kupendelea kula zaidi vyakula vya kisasa badala ya mbogamboga na matunda.

Ivomedaa alisema lishe ina nafasi kubwa katika kuathiri kiwango cha damu mwilini, hivyo ulaji wa vyakula mchanganyiko hasa mboga za majani huusaidia mwili kuzalisha damu ya kutosha ingawa ni lazima pia wajawazito wakumbuke kuanza kliniki mapema ili wapatiwe elimu ya afya ya uzazi itakayowawezesha kuishi kwa tahadhari.

Pia aliwashauri mabinti wadogo kuepuka mimba za utotoni kwa kuepuka ngono, ama kutumia vizuia mimba kwani viungo vyao vinapokuwa havijakomaa huwalazimu wajifungue kwa upasuaji na kusababisha kupoteza damu nyingi na hatimaye kuongeza mahitaji ya damu.

Ivomedaa alisema Kanda ya Ziwa yenye mikoa sita ina uhitaji wa lita 134,000 za damu kwa mwaka, ambapo mwaka huu kumekuwa na changamoto ya kupata damu ya kutosha kwa sababu ya janga la corona ambapo wachangiaji damu hawakuweza kufanya hivyo.

Aliwashauri Watanzania wote hasa wanaume kuendelea kujitolea kuchangia damu kwani wao wanaruhusiwa kuchangia kila baada ya miezi mitatu tofauti na wanawake ambao changamoto za kimaumbile, ujauzito na unyonyeshaji zinawafanya waruhusiwe kuchangia damu kila baada ya miezi minne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles