30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

WAJAWAZITO WAJIFUNGUA KWA VIBATARI, NDOO ZA MAJI

 

Na MWANDISHI WETU, Sumbawanga

WAJAWAZITO wanaokwenda kujifungua katika zahanati ya Kijiji cha Chipu, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wanalazimika kubeba ndoo za maji kichwani na vibatari kwa vile zahanati hiyo haina umeme.

Mganga Mkuu wa zahanati hiyo, Gasper Kachinga, alisema hayo juzi wakati akipokea msaada wa vitanda viwili vya kujifungulia vilivyotolewa na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, ambavyo thamani yake ni Sh milioni 2.5.

Kutokana na kukosekana kwa huduma za maji na umeme katika zahanati hiyo, wagonjwa huagizwa  kwenda na vibatari na ndoo za maji waweze kupata huduma.
Zahanati hiyo ilikuwa na kitanda kimoja cha kujifungulia wakati wagonjwa wengine hulala sakafuni au kupeana zamu.

Hilaly alisema kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji vitakavyonufaika na mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 2.1 na kwamba mkandarasi tayari amepatikana na yupo katika hatua za awali za kuanza utekelezaji.

Akizungumzia ukosefu wa umeme, mbunge huyo alisema kero hiyo itakwisha katika muda mfupi kuanzia sasa  kwa vile Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) limeanza mchakato wa kufikisha umeme kijijini hapo.

Alisema wakati huduma ya umeme ikisubiriwa, atanunua taa maalumu ambazo zitatumika katika zahanati hiyo kuwasaidia kina mama hao wasiendelee kujifungua kwa vibatari.

Hilaly aliushauri uongozi wa kijiji hicho kuweka utamaduni wa kuvuna maji ya mvua, hasa wakati wa kipindi hiki cha masika kupunguza uhaba wa maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles