Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali inatarajia kuanza kutoa virutubisho vya madini chokaa kwa wajawazito ili kupunguza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba na kujifungua kabla ya wakati.
Mwaka 2011 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa mwongozo unaoelekeza wajawazito wanaoishi katika nchi zinazopata kiwango kidogo cha madini hayo kutoka kwenye vyakula wapewe katika mgawanyo wa dozi tatu kwa siku katika kipindi chote cha ujauzito lakini Tanzania ilikuwa bado haijaanza utekelezaji huo.
Hata hivyo, Taasisi ya Afya ya Jamii ya Afrika (AAPH) kwa kushirikiana na watafiti wengine wamekuja na matokeo yanayoonyesha dozi ndogo ina matokeo sawa na dozi kubwa.
Matokeo hayo yametangazwa leo Januari 19,2024 wakati wa kongamano la tano la kisayansi lenye lengo la kubadili tafiti za afya kwa vijana wa rika balehe na lishe kuwa za vitendo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa AAPH, Dk. Mary Sando, amesema utafiti huo wa miaka mitano ulioongozwa na Chuo Kikuu cha Havard cha Marekani, ulihusisha wajawazito 11,000 kutoka Tanzania na 11,000 kutoka India kuangalia kama kuwapatia miligramu 500 za virutubisho vya madini chokaa kunaweza kuleta matokeo sawa na kuwapatia miligramu 1,500.
“Kuna kazi kubwa ya kufanya kuongea na wadau mbalimbali ili kuona tunawezaje kuweka miongozo ambayo itasaidia kuanza kutumia madini chokaa na kupunguza hatari ya mama mjamzito kupata kifafa cha mimba na kujifungua mapema.
“Watoto wanaozaliwa kabla ya muda huwa wanapata changamoto ikiwemo vifo, kifafa cha mimba ni sababu namba mbili ya kusababisha vifo vya wajawazito,” amesema Dk. Sando.
Waziri wa Afya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, Ummy Mwalimu, amesema watatumia tafiti hizo kufanya maamuzi ya kisera ingawa yameonyesha kuna gharama katika kutoa dozi hiyo kwa wajawazito.
“Hivi sasa wajawazito wote wanapewa bure na Serikali madini ya ‘folic acid’ na chuma ambayo yanawasaidia kutozaa watoto wenye vichwa vikubwa, wenye mgongo wazi na kuwaongezea damu. Watafiti wanatuambia sambamba na madini haya tuongeze ya calcium (chokaa) kwahiyo, tutalifanyia kazi na kuja na hatua za kisera kwa kuzingatia matokeo ya tafiti zilizofanywa na wanasayansi,” amesema Ummy.
Balozi wa Marekani, Dk. Michael Battle, amesema wataendelea kuiunga mkono Tanzania katika kupambana na changamoto za vijana na masuala ya afya.
Tafiti zinaonyesha dalili za kifafa cha mimba huwapata asilimia 8 ya akina mama wajawazito na inakadiriwa kusababisha zaidi ya vifo 45,000 vitokanavyo na uzazi kila mwaka. Kwa Tanzania kifo kimoja kati ya vitano vya uzazi husababishwa na kifafa cha mimba