30.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAJAWAZITO 300 WAFARIKI KWA MIAKA MITATU TABORA

Na MURUGWA THOMAS-TABORA


IMEELEZWA kuwa wajawazito 319 walipoteza maisha mkoani Tabora katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutokana na sababu mbalimbali za uzazi, huku wakisababisha vifo vya watoto wachanga 917.

Hayo yamebainishwa juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya uzazi salama na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri katika taarifa yake iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Siami Mbati, ambaye alisema kati ya vifo hivyo 23 vilitokana na mimba za utotoni.

Akisoma taarifa iliyoandaliwa na mkuu wa mkoa, Siami alisema vifo vyote vya wazazi na watoto wachanga ni tatizo la wote siyo kuachia watumishi wa afya peke yao.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 wajawazito 117 walifariki dunia, mwaka 2015 waliofariki walikuwa 107 na mwaka jana walifariki wengine 95 wakiwamo wale waliopata mimba za ututoni.

Taarifa hiyo ya mkuu wa mkoa ilizitaja sababu  za vifo hivyo kuwa ni kutokwa damu nyingi, kuwa mbali na vituo vya huduma na upungufu mkubwa wa damu, kutokuwepo kwa maandalizi ya mpango binafsi, shinikizo la damu na kupasuka mfuko wa uzazi.

Alisema kuwa vifo hivyo vinazuilika hivyo alitoa wito kwa wananchi wote kuzuia uzazi wa majumbani, mimba na ndoa za utotoni kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto.

Amebainisha kuwa  katika kufanikisha hilo kuwepo na mikakati ya kudhibiti vifo hivi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na ubia kati ya serikali na sekta binafsi kama njia mojawapo ya kuongeza ufanisi.

Awali  katika risala iliyosomwa na mratibu  wa uzazi salama Kanda ya Magharibi, Martha Mlimba, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kukumbushana ili kuhakikisha ubebaji mimba na uzazi unakuwa salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles