23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

WAJASIRIAMALI WANAZO FURSA NYINGI UCHUMI WA VIWANDA

Na Mwandishi Wetu


TUKISEMA kama Taifa tuwe na uchumi wa viwanda, watu wengi tunakuwa na fikra potofu vichwani mwetu kwa kuwa na taswira ya viwanda vikubwa vinavyotumia teknolojia ghali na kuhitaji mitaji mikubwa na hivyo kufuta uwepo wa ujasiriamali kwenye uchumi.

Ujasiriamali utaendelea kuwepo kwani kila shughuli itakayofanyika itahitaji mchanganyiko wa wawekezaji ili kufanikisha ukuaji wake.

Uchumi wa viwanda unaweka mkazo wa uzalishaji viwandani katika viwanda mbalimbali  na kwa viwango tofauti na uwezo unaotegemea uwekezaji wa mtu, kampuni na tasisi yenyewe.

Tukielekea kwenye uchumi wa viwanda, kuna mambo mengi yanatarajiwa kutokea  kwa Taifa  kwani utamaduni mpya wa maisha na tunavyoendesha mambo yetu utazaliwa.

Hivyo, utakuwa ni wakati wa kulipokea Taifa jipya lenye uwekezaji wa aina yake kwenye sekta mbalimbali za viwanda na biashara  kiwani vyote huenda sawia kwa kuleta maendeleo ya jumla ya viwanda.

Wajasiriamali wadogo na kati wanatakiwa kujiandaa vizuri kupokea ujio wa fursa kemkem zitakazoanzishwa na viwanda.

Zipo athari nyingi chanya kwa biashara ndogo na kati kutokana na viwanda hivyo ambazo zitakuwa misingi mizuri ya kuimarisha miradi iliyopo.

Viwanda huja na teknolojia mpya na hivyo kutakuwa na urahisi wa kujifunza na kutumia teknolojia za kisasa kwenye uzalishaji kwa kipindi ambacho tutakuwa na viwanda vingi vya ndani vitakavyopunguza gharama kwa wafanyabiashara watakaofungua macho.

Wajasiriamali wadogo wafanye juhudi kujiweka kwenye nafasi ya kujifunza mbinu zitumikazo kwenye uzalishaji, usambazaji na kuona wanavyoweza kutumia teknolojia hiyo kutanuka na kukuza biashara zao ili ziwe bora zaidi.

Viwanda huongeza ushindani sokoni kutokana na wingi wa bidhaa bila kujali kama zinafanana au hapana. Uwapo wa viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa tofauti utaongeza ushindani kwani wateja waliopo watatakiwa kutumia kipato chao kukidhi mahitaji yao tofauti.

 Hivyo, ubora na huduma kwa wateja ni miongoni mwa sababu zitakazowavutia na zikiwa tofauti ni muhimu na itakuwa sababu ya msingi. Wajasiriamali ndio husababisha tofauti hizo kwani ni rahisi kwao kubadilisha mambo.

Viwanda hivi pia vinaweza vikatafuta mawakala au zikawa na ofisi za kuuza bidhaa zao moja kwa moja, hivyo kuongeza ushindani kwa wafanyabiashara wadogo ambao mara nyingi huuza kwa bei ya juu.

 

Kuimarika kwa bei za malighafi

 

Kisera Serikali inalazimika kuhamasisha matumizi ya malighafi za ndani kwa ajili ya ongezeko la thamani na kulinda ajira za wananchi, huku ikizuia zile za nje. Wakulima na wafugaji wa mashambani watapata stahiki zao kwani wanakuwa na uhakika wa soko na kuepukana kupunjwa na walanguzi wa soko. Hali hiyo huleta ustawi kwa wananchi wengi.

Bidhaa na huduma zilizoongezwa thamani ya masoko yote mawili; ndani na kimataifa. Viwanda vitakuza na kuboresha bidhaa na huduma na kuwa kwenye nafasi ya kujifunza na kukubali mabadiliko kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma.Tutatengeneza biashara zenye nguvu na kwa masoko ya uhakika.

Ujaji wa viwanda utaandamana  na kutanua masoko ya huduma na bidhaa za viwandani nje ya Tanzania  na Afrika Mashariki  na mbali zaidi. Ni fursa kwa wajasiriamali kuangalia hili na kuanza kujiandaa na ujio wake kwa kuchangamkia fursa za masoko makubwa ndani na nje kwa ustawi wa biashara.

Uwepo wa viwanda huashiria ukuaji uchumi na huelekeza  ustawi na kutanuka kwa huduma za taasisi za fedha kutokana na msukumo utakaokuwapo kutokana na shughuli za viwanda vitakavyojengwa kwa kuongeza mahitaji na mzunguko wa fedha.

Watu na taasisi za viwanda huhitaji na hutumia huduma za fedha na hivyo zitakuwa muhimu kwa wafanyakazi viwandani  na watumiaji wa bidhaa zake.

Ni muhimu kwa Watanzania kujiandaa kupokea mabadiliko haya yatakayokuwa na tija katika  kila sekta  na hivyo kuongeza shughuli nyingine za ujasiriamali kutokana na mahitaji husika.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,314FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles