Na Clara Matimo, Mwanza
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza, linatarajia kusherekea sikukuu ya Idd El Hajji Julai 21 mwaka huu kwa kuwafundisha waumini wa dini hiyo kuhusu umuhimu wa kutoa zaka.
Pamoja na somo hilo pia viongozi wa dini hiyo watawafundisha waumini wao kuhusu umuhimu wa afya, umoja miongoni mwao na kuwajulisha mipango ya maendeleo ya miezi mitatu iliyowekwa na uongozi wa bakwata mkoani humo.
Hayo yameelezwa leo na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, alipozungumza na Mtanzania Digital ambapo alifafanua kwamba baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu bado hawajatambua umuhimu wa kutoa zaka wakati ni miongoni mwa nguzo tano za uislamu.
Alisema ni wajibu wa viongozi wa dini hiyo kuwafundisha waumini wao ili waelewe vyema nguzo tano za uislamu ambazo ni shahada, swala, zaka, kufunga na hija lakini kupitia sikukuu ya Idd El Hajji watajikita kuwafundisha kwa kina kuhusu nguzo ya tatu.
“Zaka ni nguzo ya tatu katika dini ya uislamu ambayo imeagizwa na Mwenyezi Mungu kupitia kitabu kitakatifu cha Quran, kila muislamu hutakiwa kutoa vitu mbalimbali ikiwemo mali, biashara, madini na wanyama kwa kadri Mungu alivyombariki lakini je ni kweli wote tunatekeleza hili kwa moyo mkunjufu na kwa uaminifu? Alihoji na kuongeza.
“Kama muislamu asipoisimamia misingi ya dini yake si jambo jema na sisi viongozi wao wajibu wetu ni kuwafundisha kwa kina waelewe ili mtu asipotimiza iwe ni kwa utashi wake mwenyewe siku ya kiama asije akajitetea kwamba viongozi wangu hawakunifundisha.
“Lakini yawezekana wengine hawatoi kwa sababu hawajui faida za kutoa zaka labda walifundishwa hawakuelewa vizuri tunaamini tukiwafundisha kwa kina kuhusu faida za kumtolea mwenyezi Mungu zaka hawataacha maana kila mwanadamu anapenda Mwenyezi Mungu ambariki,”alieleza.
Akizungumzia elimu ya afya, Sheikh Kabeke amewataka waumini wa dini hiyo kuendelea kufuata maelekezo ya Serikali katika kujikinga na ugonjwa wa korona pia kila mtu atambue umuhimu wa kakata bima ya afya ili awe na uhakika wa matibabu atakapougua.
Kuhusu umoja miongoni mwao, Sheikh huyo amesema wanaendelea kuwafundisha waumini wao ukarimu, mshikamano na upendo ili waendelee kuishi kwa kuthaminiana na kuheshimiana.
“Hatuhitaji kuona tofauti za mitazamo ama itikadi zinafarakanisha waislamu, kwenye uislamu yapo madhehebu mengi lakini wote ni waislamu hivyo kupitia siku kuu ya Idd El Hajji tutaendelea kuwafundisha waumini wetu umoja,”alisema Sheikh Kabeke na kuongeza.
“Tumeanza mchakato wa kutengeneza mtandao wa kumbukumba za waislamu yaani data bese, tunaamini mfumo huo ukikamilika utatusaidia sana kupanga mipango ya maendeleo, tulikwisha zindua mfuko wa maendeleo ya bakwata wa mkoa wetu lengo letu ni kuwaletea waislamu maendeleo katika sekta mbalimbali,”alisema.
Sheikh Kabeke amesema swala ya sikukuu ya Idd El Hajji itafanyika kimkoa katika uwanja wa Nyamagana uliopo jijini hapa ambapo amewataka waislamu kuonyesha ukarimu kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji wakiwemo wajane na yatima ili nao waweze kusherekea kwa kula na kunywa vitu vilivyoharalishwa na Mwenyezi Mungu kama alivyofundisha Mtume Mohamed(swa).