24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wahasibu, makatibu Amcos Simiyu wapigwa msasa kupunguza hati chafu

Na Derick Milton, Simiyu

Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (TFC) kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa vyama vya ushirika (COASCO), wameendesha mafunzo ya siku nne kwa watendaji wa vyama vya ushirika Mkoa wa Simiyu ya namna bora ya uandishi wa vitabu vya fedha.

Hatua hiyo inatokana na asilimia 80 ya vyama vya ushirika katika mkoa huo kupata hati chafu wakati wa ukaguzi huku asilimia 20 vikipata hati yenye mashaka na isiyoridhisha.

Mhasibu wa shirikisho hilo la vyama vya ushirika, Christian Mkunde, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa uwepo wa hati nyingi chafu ndicho chanzo kilichowasukuma kutoa mafunzo hayo.

Amesema kuwa wamegundua kuwa chanzo cha hati chafu, kinatokana na wahusika katika uandishi wa vitabu vya fedha ambao ni wahasibu na makatibu baadhi yao kukosa ujuzi na uwezo wa kujaza vitabu hivyo.

Mkunde ameeleza kuwa kutokana na uwezo wa vyama vya msingi vya ushirika, vingi vimekuwa vikiajiri watu wa kawaida wakiwemo wenye elimu ya darasa la saba au kidato cha nne kuwa wahasibu na makatibu bila ya kuwa na taaluma.

“Lakini baadhi ya vyama kutokana na wahasibu au makatibu wake kukaa muda mrefu bila ya kupata mafunzo ya mara kwa mara, wamekuwa wakisahau jinsi ya kujaza vitabu kwa usahihi.

“Ndiyo maana kama Shirikisho kwa kushirikiana na COASCO, tukaamua kuja kuwapiga msasa wa kuwakumbusha jinsi ya kujaza vitabu hivyo na kuwaonyesha wapi wamekuwa wakikosea,” amesema Mkude.

Rodrick Kilemile kutoka COASCO mkoani Shinyanga, amesema kuwa wahasibu na makatibu wengi katika vyama vya ushirika wamekuwa wakisahau kujaza vitabu licha ya wengi kuwa na uzoefu wa muda mrefu.

Amesema kuwa katika ukaguzi ambao wamekuwa wakifanya kila mwaka, tatizo kubwa wengi ni kusahau lakini wapo baadhi hawajui jinsi ya kujaza huku wengine pindi wanapomaliza vitabu ulazimika kwenda kujaza kwenye madaftari yao ya kawaida.

“Tumegundua kuwa baadhi ya Amcos hazina vitabu vya kutosha, vitabu wanavyo vichache, sasa wanapomaliza vitabu wanaamua kuandika taarifa za fedha kwenye vitabu vya kawaida, hali ambayo usababisha kupata hati chafu,” amesema Kilemile.

Awali, akifungua mafunzo hayo Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoa, Ibrahimu Kadudu amesema kuwa kwa Mwaka 2021 jumla ya vyama vya msingi 375 vilikaguliwa kati ya vyama 379, ambapo 166 kati ya hivyo vilipata hati mbaya, 157 hati isiyoridhisha na 52 vilipata hati yenye mashaka.

Kadudu amesema kupitia mafunzo hayo, wahasibu na makatibu watajifunza namna bora ya kuandaa vitabu vya fedha kwa kufuata kanuni na taratibu za uadishi wa taarifa za fedha na kuondokana na hali ya kupata hati chafu.

Aidha, amevitaka vyama hivyo kuhakikisha wanafanyia kazi hoja zote za ukaguzi na kujibiwa kwa ufasaha na kwa wakati, kwani zimekuwepo na hoja nyingi ambazo hazifanyiwi kazi hali ambayo imesababisha kupata hati chafu.

Maria Lucas Mhasibu kutoka Amcos ya Duluma, ameishukuru TFC pamoja na COASCO kwa kuwaletea mafunzo hayo, kwani tatizo kubwa kwao ni kusahahu baadhi ya vitu wakati wa kujaza vitabu hivyo.

Katibu huyo amesema kuwa kushindwa kujaza vyema vitabu hivyo, imekuwa ikisababisha kukamatwa na kufungwa kwa madai ya kuiba fedha za wakulima jambao ambalo wakati mwingine siyo kweli bali ni kutokana na kutojaza vyema vitabu hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles