30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wahariri waomba miezi 3 kujadili muswada wa habari

Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo
Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa habari nchini, wameiomba Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma za Jamii kutoa miezi mitatu kwa wadau wa sekta hiyo ili waweze kuujadili kwa kina Muswada wa Sheria ya Habari wa mwaka 2016.

Hayo yamekuja kutokana na kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba kutoa wiki moja kwa wadau kuujadili muswada huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa TEF, Neville Meena, alisema kama wakipewa muda huo hadi Februari, mwakani, watapata fursa nzuri ya kujadili muswada huo.

Alisema ndani ya muda huo, wataweza kujadiliana na kupata majibu sahihi na mazuri kwa ajili ya mustakabali wa waandishi wa habari na wadau kwa ujumla.

“Kwa muda wa miezi mitatu, tutakuwa tumefanya majadiliano, tukumbuke kila taasisi ina wadau wake, lazima wakae na kujadilina na ukifika muda huo tutakuwa tumepata majibu mazuri,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema muswada huo ni muhimu kwani sio kwa ajili ya waandishi tu, bali hata wananchi nao unawahusu.

“Muswada huu ni muhimu, naomba tuongezewe muda wa majadiliano, haupo kwa ajili ya waandishi tu, hata wananchi unawahusu. Kuna vipengele tunatakiwa tujadiliane kabla ya kuwa sheria.

“Tunataka sheria ambayo haitamwonea mtu pamoja na kumwogopa, tunataka itende haki kwa kila mmoja, tunaomba tupewe muda hadi Februari mambo yatakuwa yamekaa vizuri,” alisema.

Naye Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo, alisema waandishi wengi wa habari bado hawajaupitia muswada huo, hivyo kama watapata muda huo utawasaidia kujadiliana.

Alisema kuna klabu 27 za waandishi wa habari, huku kukiwa na zaidi ya wanahabari 2,000 ambao wengi wao hawajausoma.

Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), John Seka, alisema kuna umuhimu wa kupata muda wa ziada kutokana na wadau kuiomba sheria hiyo kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Henry Muhanika, alisema muda huo wameomba wao wenyewe, hivyo watafanya kulingana na muda walioomba.

Awali katika Ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani hapa, kuliibuka mvutano kati ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) baada ya kupishana kimtazamo kuhusu kupokea maoni ya wadau katika muswada huo.

Sintofaamu ilianza baada ya Serukamba kusoma maudhui ya sheria hiyo pamoja na mchakato wake katika hatua zote na baada ya kumaliza akataka wadau waanze kutoa maoni yao hali iliyomuibua Zitto.

“Hapa yupo (Nape Nnauye), ningependa atusaidie kujua kama wadau walipata muda wa kushirikishwa kikamilifu na kuwapa nafasi nzuri ya kutoa maoni yao,” alisema Zitto.

Kauli ya mbunge huyo ilipokewa kwa shangwe na wabunge walioiunga mkono, lakini baadhi wakaanza kupinga na kufanya ukumbi huo kutawaliwa na kelele.

Huku akisisitiza kuwa yuko sahihi kuhusu namna ya uendeshaji wa vikao, Serukamba alijikuta akipingwa na kila mtu hata akaanza kumlalamikia Zitto kuwa anasimama upande wa wadau wakati yeye ni mbunge.

Lakini, Zitto akajibu kwa sauti kuwa wapo wapigakura wake kutoka Kigoma mjini wanahusika na muswaada huo.

Alipopewa nafasi Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alisema anaungana Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles