26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAHARIRI WAMWEKA NJIA PANDA PROFESA LIPUMBA

Mwandishi wa Gazeti la MTANZANIA, Asha Bani, akilia wakati wa akielezea namna walivyopigwa kwenye mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) katika mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri (TEF) kwa ajili ya kulaani tukio hilo, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa jukwa hilo, Theophil Makunga.

 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF)  limemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, atoe kauli kuhusu tukio la kushambuliwa na kuumizwa kwa waandishi wa habari.

TEF imesema tukio hilo linaingilia uhuru wa habari na ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kwamba wanalitazama kama shambulio dhidi ya uhuru wa habari na waandishi wa habari nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema baada ya tukio hilo walizungumza na pande mbili zenye mgogoro ndani ya CUF ambako Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad aliandika barua kwa jukwaa hilo akilaani kupigwa kwa waandishi hao.

Alisema pia mwanzoni mwa wiki hii, walifanya mawasiliano na Profesa Lipumba   kupata kauli yake kuhusu kilichotokea lakini hadi sasa hajaweka bayana msimamo wake.

“Tumebaini kuwapo  viashiria kwamba mashambulio dhidi ya waandishi wa habari yalifanywa na kundi la watu wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.

“Mmoja wa wafuasi wake, Abdul Kambaya, jana (juzi) alizungumza na waandishi wa habari na kukiri kwamba vurugu zile zilifanywa na vijana wa CUF huku akiomba radhi kwa yaliyotokea,” alisema Makunga.

Hata hivyo alisema mkutano huo wa Kambaya ulighubikwa na matukio kadhaa yakiwamo ya ubaguzi wa vyombo vya habari na viashiria vilivyotishia usalama wa waandishi wa habari.

“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mikutano ya habari ya Profesa Lipumba na wafuasi wake. “Hatujafikia hatua ya kuzuia kuripoti habari zake, tunampa nafasi kwanza, anaelewa msimamo wetu, ikiwa hatutaridhika na hali ya usalama kwa waandishi wa habari tutalazimika kuchukua hatua zaidi.

 “Tunatoa wito kwa wahariri na waandishi wa habari wachukue tahadhari ya hali ya juu wanapoitwa kuripoti mikutano ya kundi hili la siasa,” alisema.

Jukwaa hilo pia limelitaka Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo na kuchukua hatua za sheria dhidi ya wahusika wa uhalifu huo.

“Tunasema hivi tukirejea kukamatwa kwa mmoja wa watuhumiwa katika eneo la tukio, tunatoa wito kwa umma wa Watanzania kutambua kwamba waandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Makunga .

Alisema licha ya mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa fursa ya kuandikwa na kutangazwa   habari za pande zote mbili zinazovutana, hivyo kitendo cha kuwashambulia waandishi wa habari hakivumiliki na hakikubaliki.

Alisema vitendo vya kuwapiga na kuwabughudhi waandishi wa habari havipaswi kupewa nafasi nchini kwa sababu  vinawanyima wananchi haki ya kupata taarifa kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 18 (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Katibu wa TEF, Neville Meena, alivitaka vyama vya siasa nchini vijenge ustaarabu na kuaminika na kuhakikisha mikutano yao inakuwa salama.

“Kwani ni lazima tuandike habari za CUF ndiyo magazeti yauzwe?  CUF wajue kwamba wako kwenye uangalizi na uamuzi unaweza kutolewa wakati wowote,   lazima tuhakikishe watu wetu wanakuwa salama,” alisema Meena.

Pia aliwaasa waandishi wa habari kuwa na umoja bila kujali tofauti zao na kuacha kutetea uovu uliofanyika hadharani.

 

WAANDISHI WAANGUA VILIO

Katika mkutano huo waandishi ambao walikuwa wakitekeleza wajibu wao taaluma kisha kushambuliwa na kupigwa, walieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea na namna walivyojaribu kujinasua.

Mmoja wa waandishi hao, Fred Mwanjala (Channel Ten), alisema mpango wa kuwashambulia ulikuwapo kwa sababu licha ya kujitambulisha bado waliendelea kushambuliwa na kupigwa.

“Nia ya kutushambulia ilikuwapo kwa sababu walikuja mara ya kwanza wakafungua mlango, wakachungulia halafu wakaja mara ya pili ndiyo wakaanza kutushambulia.

“Mimi nilikuwa nimekumbatia kamera isiharibiwe hivyo katika kujitetea nikajikuta nimeanguka na kuumia mkono wa kushoto.

“Tunasikia nchi mbalimbali Somalia, Afrika Mashariki na Kati na kwingineko waandishi wenzetu wanauawa na sisi hatuwezi kukaa kimya,” alisema Mwanjala.

Naye Asha Bani wa gazeti hili, alisema anashangazwa na vyombo vya dola kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote hadi sasa licha ya wao kuumizwa.

 “Sisi tumeumizwa na hakuna zilizochukuliwa mpaka sasa, jeshi la polisi limekaa kimya, Waziri wa Habari, Waziri wa Mambo ya Ndani wote wamekaa kimya.

“Matokeo yake jana (juzi) wametupigia simu wanaanza kututisha…tunazidi kunyanyasika kwenye maeneo yetu ya kazi,” alisema Asha huku akilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles