27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

WAHARIRI WACHAMBUA VIKWAZO VYA KUPATA HABARI

Na MWANDISHI WETU-DODOMA


JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limechambua vikwazo vinavyosababisha upatikanaji wa habari, huku wakitaka kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa uhuru wa habari nchini.

Akisoma hotuba ya jukwaa hilo mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na wadau wengine wa habari jijini hapa jana, Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na mazingira magumu ya kazi kwa wanahabari.

Alisema baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola wamekuwa wakiwabughudhi wanahabari wanapokusanya habari.

“Waandishi wamekuwa wakinyang’anywa simu zao, kuwekwa chini ya ulinzi na kuachiwa bila kufikishwa mahakamani, hivyo kuwatia wasiwasi wa kudumu.

“Tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, aliyepotea Novemba 29, mwaka 2017, ambaye hadi leo hajulikani alipo, limeongeza hofu kwa waandishi wa habari, hasa wale wanaoripoti habari za uchunguzi.

“Vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa na mamlaka kama Idara ya Habari – Maelezo kwa magazeti na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA kwa vyombo vya kielektroniki.

“Na wakati mwingine kupewa adhabu kubwa za kulipa faini ama kufungiwa kama ambavyo hivi karibuni vituo vya televisheni vya Star TV, ITV, Azam, EATV na Channel 10 vimepigwa faini ya Sh milioni 65 na kuwekwa chini ya uangalizi kwa kutangaza habari zilizotokana na ‘press conference’ iliyoitishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kuvituhumu eti ‘haviku-balance’ habari hiyo.

“Hivi TCRA wanapotuita waandishi na kutueleza mpangilio wa masafa au baadhi ya vituo kunyang’anywa masafa, mbona huwa tunatangaza habari hizo na hatupigwi faini kwa ‘kuto–balance’ kwa walionyanganywa masafa? Nchi yetu imefika huko kweli?

“Kuna kundi au watu wanaoitwa wasiojulikana, wameleta hofu kubwa miongoni mwa waandishi wa habari, kwa kiwango ambacho katika historia ya nchi hii tumeshuhudia mwandishi Ansbert Ngurumo akikimbilia nje ya nchi kwa maelezo kuwa watu wasiojulikana walikuwa mbioni kuhatarisha maisha yake.

“Tukio la kuzuia Bunge ‘Live’, ambalo lilianza rasmi mwaka 2016, limeendelea kuwapo na kuwakosesha wananchi haki ya kupata habari.

“Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, amekuwa akitumia vibaya kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, kinachompa mamlaka ya kuzuia maudhui, lakini yeye amekitumia kwa nyakati tofauti kufungia magazeti kama Mawio, Mwanahalisi, Mseto, Tanzania Daima na Raia Mwema.

“TCRA kupitia kwa waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, imetunga kanuni za kudhibiti mitandao ya kijamii za mwaka 2018, ambazo kiuhalisia hazitekelezeki, zinatoa majukumu na wajibu, ambavyo ni vya kikampuni kwa mtu ambaye anaanzisha blog kuwasiliana na ndugu na jamaa, jambo linalokiuka haki za msingi za binadamu.

“Yamekuwapo matukio ya watendaji wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuviandama vyombo vya habari vinavyofanya kazi ya kuonyesha kinachoendelea wakati wa uchaguzi. Kwa mfano kuibwa na kurejeshwa kwa sanduku la kura pale Kinondoni, waandishi kuitwa na kuhojiwa bungeni na mengine mengi,” alisema Balile.

Alisema kutokana na matukio hayo, wamebaini kuwapo hali ya kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini na matukio ambayo hayana afya kwa taifa huko tuendako, huku akitolea mifano ya nchi nyingi duniani ambazo ziliingia katika gharama kubwa ya watu wake kwa kudharau matukio madogo madogo kama ambayo yanatokea hapa nchini.

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles