24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wahariri gazeti la Mawio wahojiwa kwa saa nne

Pg 3 jan 19Na Wandishi Wetu, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewahoji wahariri wa gazeti la Mawio ambalo limefutwa kwa muda wa saa nne mfululizo.

Hatua ya kuhojiwa kwa wahariri hao inatokana na agizo la jeshi hilo kuwataka kujisalimisha kwa hiyari.

Aliyekuwa wa kwanza kuhojiwa ni mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa, ambaye alisema katika mahojiano yao alitakiwa kueleza namna alivyopata chanzo chake cha habari kuhusu habari ya urais wa Zanzibar.

Alipoulizwa kama ametaja chanzo hicho, Idrisa alisema hajataja kwani sheria na maadili ya habari hairuhusu kufanya hivyo.

“Nimehojiwa kuhusu chanzo cha habari yangu niliyoandika kuhusu Zanzibar na chanzo changu kama ni Tundu Lissu ama la, lakini jibu nilisema si Tundu Lissu… hata hivyo nikawajibu muulizeni mwenyewe kwa sababu ni mwanasheria na mwanasiasa anaweza kujieleza vizuri zaidi,” alisema Idrisa.

Mwingine aliyehojiwa ni mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina ambaye hadi tunakwenda mitamboni alikuwa bado anaendelea na mahojiano na makachero hao wa Jeshi la Polisi.

Idrisa alikuwa wa kwanza kufika kituoni hapo saa 8:56 mchana akiambatana na mwanasheria wa Mawio, Frederick Kihwelo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea pamoja na aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo.

Baada ya kufika aliingizwa katika Ofisi ya Kamanda Sirro kwa ajili ya mahojiano ambapo waandishi wa habari na alioongozana nao walifukuzwa na kuambiwa watoke katika eneo hilo kwani hawahusiki.

Ilipofika saa 9:15 alasiri Mkina aliwasili katika kituo hicho na kwenda moja kwa moja katika ofisi hiyo ambapo aliambiwa asubiri nje hadi muda wake utakapofika.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili kituoni hapo, Mwenyekiti wa TEF, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alisema yeye ni mwenyekiti wa TEF amekuja kumsindikiza mhariri mwenzao polisi hapo lengo ni kujua walichoitiwa na kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru.

“Tumekuja kuwasindikiza wenzetu hawa kwakuwa ni wajumbe wa TEF, pia kujua sababu gani ya polisi kuwaita wahariri hawa… tumesikia polisi inawatafuta wahariri wa Mawio,” alisema Kibanda.

Kibanda alitumia nafasi hiyo kutoa masikitiko yake kwa hatua iliyochukuliwa na Serikali kwa kulifungia gazeti la Mawio.

Alisema Serikali inanyima uhuru wa habari kwani wao TEF hawaoni kosa walilofanya gazeti hilo hadi kutoa adhabu hiyo kubwa.

“Tumesikitika sana na hatua hii ya kikandamizaji ya kulifungia gazeti la Mawio na huu ni mwendelezo wa Serikali kunyima uhuru wa habari nchini, na sisi Jukwaa la Wahariri hatutakubali kufanya kazi na waziri wa aina hii na tutatoa tamko,” alisema Kibanda.

Gazeti la Mawio lilifungiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kusema kuwa gazeti hilo lilikuwa linaandika habari za uchochezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles