Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Wahandisi nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, nidhamu, na uwajibikaji ili kuhakikisha taaluma hiyo inatoa mchango stahiki katika maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo, Februari 11, 2025, na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, wakati wa semina ya 18 ya utangulizi kwa wahandisi 362 waliojiandikisha katika Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo (SEAP).

Amesema semina hiyo inalenga kuwajengea msingi imara wahandisi wapya ili waweze kutimiza malengo ya bodi kwa ufanisi.
“Mafunzo haya hufanyika kila mwaka ambapo tunawaelekeza wahandisi kufanya kazi kwa kuzingatia miiko na maadili yaliyowekwa na bodi,” amesema Kavishe.
Katika hafla hiyo, wahandisi zaidi ya 200 waliapa kiapo cha uadilifu, huku Kavishe akisisitiza kuwa bodi ina jukumu la kuhakikisha wahandisi wanakua kitaaluma tangu wanapohitimu hadi wanapostaafu.
Akifungua mafunzo hayo, Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ECI) kutoka India, Dk. Priya Swarup, amesema India na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu na wataendelea kushirikiana katika kuboresha sekta ya uhandisi.

“Sisi ni marafiki wa muda mrefu, na tutaendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuwajengea uwezo wahandisi wa Tanzania,” amesema Dk. Swarup.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Asha Mahimbo, amesema semina hiyo itawawezesha wahandisi kujua mahitaji ya soko la ajira na kufuata sheria na taratibu za taaluma hiyo.
“Tunalenga kuhakikisha tunaendana na vigezo vya kitaaluma ili taaluma yetu iwe na tija kwa taifa,” amesema Mahimbo huku akihamasisha wasichana kujitokeza kusoma masomo ya sayansi.

Naye Mhandisi Andrew Mongella, aliyeshiriki katika kiapo cha uadilifu, amesema kiapo hicho kinawaweka wahandisi kwenye wajibu wa kuzingatia miiko ya taaluma na kutanguliza maslahi ya taifa katika kazi zao.
“Ni kiapo cha msingi kinachoonyesha utayari wetu wa kuhudumia taifa kwa weledi, maadili, na uwajibikaji,” amesema Mongella.