23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wahandisi kortini kwa tuhuma za rushwa

 YOHANA PAUL

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani aliyekuwa Mkuu wa idara ya Ugavi na Manunuzi, Justin Mgasa, Mkuu wa Idara ya Maji Juma Maganga, Mhandisi Mshauri Rugemalira Kazimoto na Mkurugenzi wa Kampuni ya Famoyo Contractors Ltd Yasin Mohamed Ali.

Akisoma mashitaka wiki iliyopita katika mahakama ya Hakimu Mkazi Geita mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Geita Samwel Maweda, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Augustino Mtaki alisema watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa ya Kuomba na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 239 iliyorejewa mwaka 2019.

Alisema katika kesi hiyo namba CC. 244/2020 kati ya mwezi Januari hadi Desemba 2014 washitakiwa hao wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao walipokea kiasi cha Sh milioni 410 kama hongo ili waweze kurekebisha masharti ya mkataba Na. LGA/091/NRWSSP/G/2013/2014/01 kwenye kipengele cha dhamana ya mkataba.

Alisema katika kipindi hicho mshitakiwa wa tatu na wanne wakiwa ni wakandarasi washauri wa mkurugenzi wa Famoyo Contractors aliyepewa kandarasi ya kusambaza mabomba ya maji katika vijiji vya Nyamtukuza, Kakora na Nyarubele walitoa rushwa ya kiasi cha Sh milioni 410 ukiwa ni ushawishi ili wafanyiwe marekebisho ya masharti ya mkataba huo.

Washtakiwa wote walikana makosa yote na kupewa masharti ya dhamana kwa kutakiwa kila Mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua za utambulisho na nakala za vitambulisho watakaosaini fungu la dhamana la Sh milioni 20 kila mmoja huku washitakiwa pia wakitakiwa kusaini fungu la dhamana la Sh milioni 20 kila mmoja.

Washitakiwa hao walikidhi masharti ya dhamana na kuachiliwa huru na kesi hiyo iliahirishwa mpaka agosti 13 mwaka huu itakapotajwa tena.

Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Leonidas Felix alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Geita kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika katika Ofisi ya Takukuru au kwa kupiga simu kwenda namba 113 kusaidia watuhumiwa wote kuchukuliwa hatua za kisheria ili kufanikisha kukata mnyororo wa rushwa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles