Aveline Kitomary
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza ongezeko la wagonjwa wenye maambukizi ya corona 196 nchini, Tanzania Bara ikiwa na wagonjwa 174 na Zanzibar wagonjwa 22 ambao walitolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid na kufanya idadi ya wagonjwa wa corona nchini kufikia 480.
Majaliwa amesema hayo leo Jumatano Aprili 29, jijini Dodoma wakati akigawa magari 50 ya kubebea wagonjwa kwa wabunge wa majimbo mbalimbali.
Amesema jumla ya wagonjwa waliopona imeongezeka kutoka 48 hadi kufikia 197, huku Zanzibar waliopona wakiwa 36 na Tanzania bara 83.
“Kumekuwa na ongezeko la vifo vya watu sita na hivyo kufanya idadi ya vifo vilivyotoka na corona nchini kufikia 16.
“Kati yao wenye maambukizi 297, waliobaki 283 wanaendelea vizuri na tiba na kusubiri ufuatiliaji wa afya zao na wengine 14 wako chini ya uangalizi maalumu wa madaktari ambao wanahitaji oksjeni ya kuwasaidia kupumua pamoja na wale wenye magonjwa mengine ambayo yamejitokeza kwenye wodi.
“Serikali imeendelea kuwaondoa washukiwa waliokuwa karantini ambao walishatimiza siku 14 baada ya uchunguzi wa kiafya kuonekana hawana maambukizi na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” amesema.
Majaliwa amesema hadi kufikia jana Aprili 28, watu 644 wameruhusiwa kutoka karantini katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Zanzibar, Kilimanjaro, Mwanza, kagera, Songwe, Kigoma na Dodoma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amekemea tabia ya upotoshaji na utoaji wa takwimu ambazo si rasmi na kuzua taharuki kwa jamii kwamba kila kifo kimetokana na Corona kuwa si sahihi na kusisitiza kuwa kuna magonjwa mengine ambayo yanaua pia.