23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa wa corona wafika 13

Ramadhan Hassan – Dodoma

SERIKALI imesema walioambukizwa virusi vya corona nchini wamefikia 13, huku Rais Dk. John Magufuli akisema virusi hivyo havitazua Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba wala Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Machi 31.

Katika hatua nyingine, mgonjwa wa kwanza kubainika kuwa na virusi hivyo nchini, Isabela Mwampamba (46), ameripotiwa kupona na anatarajiwa kuungana na familia yake hivi karibuni.

Wakati hayo yakiendelea nchini, kwa ujumla duniani kote hadi jana vifo vitokanavyo na virusi hivyo vilikuwa 21,000 huku watu 472,000 wakibainika kuambukizwa na 114,000 wakiwa wamepona.

Italia bado inaongoza kwa vifo, watu 7,500 wamefariki dunia ingawa kwa sasa maambukizi mapya na vifo vinashuka ikiwa ni mafanikio ya nchi hiyo yote kuingia karantini na kukataza watu wake kutoka nje ya nyumba zao.

Hispania ndiyo inayotajwa kuwa vifo vinazidi kuongezeka, kwa saa 24 hadi jana walifariki dunia watu 655 na kufikisha idadi ya waliopoteza maisha kuwa 4,100.

Hali ni mbaya Marekani nako, ambako maambukizi mapya yamefika zaidi ya 70,000 huku watu waliopoteza maisha wakiwa 1,050 wakati Uingereza ikifikisha vifo 465.

JPM UCHAGUZI PALEPALE

Jana Rais Magufuli alisema Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, hautaahirishwa licha ya kuwapo mlipuko wa virusi vya corona.

Rais Magufuli aliyasema hayo Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ripoti ya Takukuru.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri kazi hazifanyiki na hakuna kukutana hata kwa mabaraza ya madiwani na Bunge kwa sababu ya corona, na kusema hata nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo, bado mabunge yao yanakutana.

“Sisi tunaendelea kukutana, ndiyo maana hata Bunge linaendelea na vikao vyake, hata huko kwenye nchi zilizoathirika kabisa, mamilioni ya watu wamekufa kwa corona, bado mabunge yao yanakutana, kazi lazima ziendelee.

“Na uchaguzi tutafanya, wapo wanaofikiri kwamba tutaahirisha, nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo?” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia amesoma kwenye moja ya gazeti likihoji Baraza la Mawaziri kukaa wakati kuna katazo la mkusanyiko kwa sababu ya corona.

Rais Magufuli alisema kazi lazima ziendelee na mabaraza hayo yataendelea na kazi zake na hata Bunge litaendelea na kazi zake, ikiwamo kuchambua ripoti zilizowasilishwa na CAG na Takukuru.

WAGONJWA WAFIKA 13, ISABELA APONA

Jana jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wagonjwa wa virusi hivyo wamefika 13.

Alisema hadi jana watu 273 Tanzania bara na Zanzibar walichukuliwa sampuli za kupima virusi vya corona na kati ya sampuli hizo, 260 hazikuonyesha uwepo wa virusi hivyo, huku sampuli za watu 13 zilithibitika kuwa navyo.

“Mnyambuliko wa wagonjwa hao ni kama ifuatavyo: Arusha watu wawili, Dar es Salaam watu nane, Zanzibar wawili na Kagera mtu mmoja,” alisema Ummy.

Alisema katika wagonjwa hao, nane ni raia wa kigeni na watano ni Watanzania.

 “Katika ya wagonjwa hao, mmoja tu ndiye ambaye hakusafiri nje ya nchi katika siku 14 kabla ya kuthibitishwa kuugua, na huyu mgonjwa mmoja alipata maambukizi kutoka kwa mtu aliyekuwa nje ya nchi,” alisema Ummy.

Alisema mkoani Kagera amepatikana mgonjwa wa corona ambaye ni dereva wa malori yanayofanya safari zake nchi za Congo, Burundi na Tanzania.

“Lakini huyo wa Kagera aliingia nchini kupitia mpaka wa  Kabanga ambao ni kati ya Tanzania na Burundi kwa hiyo anaendesha malori Tanzania, Burundi na Congo,” alisema Ummy.

Waziri huyo aliyekuwa ameongoza na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamadi Rashid Mohammed, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile na Katibu Mkuu, Dk. Zainabu Chaula, alisema Serikali inaendelea kudhibiti virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi kwa kuwapima joto la mwili wasafiri wote wanaoingia nchini.

Alisema kuanzia Januari mosi hadi sasa, wasafiri 1,890,532 wamefanyiwa ukaguzi wa kuwapima joto la mwili katika vituo 27 vya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandarini.

“Katika masaa 24 yaliyopita (hadi jana), wasafiri 3,471 wamefanyiwa ukaguzi wa kuwapima joto huku Wizara ya Afya ikiendelea kutoa huduma za upimaji wa sampuli za washukiwa wa corona katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii,” alisema Ummy.

Alisema mgonjwa wa Arusha ambaye alijulikana kwa jina la Christabela amepona ugonjwa huo.

“Na leo (jana) nina furaha kuwajulisha kuwa mgonjwa wetu wa Arusha, wa kwanza, amepona na taratibu za kumruhusu kurudi nyumbani zinaendelea,” alisema Ummy.

WASAFIRI 245 WATENGWA

Katika hatua nyingine, Ummy alisema kuanzia Machi 23  abiria wote waliowasili nchini kutoka nchi zilizoathirika zaidi na virusi vya corona wamewekwa karantini ya lazima ya siku 14 katika hoteli na maeneo maalumu yaliyobainishwa na Serikali kwa gharama zao.

Alisema  wasafiri 111 kwa Tanzania Bara na 134 kwa Tanzania Visiwani wametegwa kwenye hoteli na maeneo yaliyoandaliwa.

“Mikoa yote nchini inaelekezwa kuendelea na zoezi la kubainisha sehemu zitakazotumika kuwaweka wasafiri na kuweka utaratibu mzuri wa kutekeleza maelekezo ya Wizara ya Afya bila kuleta usumbufu usio wa lazima kwa wasafiri.

“Hii ni pamoja na kuhakikisha wasafiri wanamudu gharama za sehemu husika na kuhakikisha wataalamu wa afya wanaendelea kutoa ushauri nasaha kwa wasafiri ili kutimiza dhamira nzuri kwa Serikali ya kupunguza hatari ya kusambaa kwa maradhi haya nchini,” alisema Ummy.

MAJINA YA WAGONJWA

Ummy alisema siku zote wataendelea kuficha siri za wagonjwa na katu hawatawataja majina labda wahusika wajitaje wenyewe.

“Sijawahi hata mara moja kutaja jina na sitataja jina, Isabela alitajwa na baadhi ya watu na mwenyewe alijitaja, Mwana Fa (mwanamuziki Hamis Mwinjuma) alijitaja mwenyewe, taratibu zinatuzuia kutaja majina,” alisema Ummy.

MALALAMIKO KUHUSU VIPIMO

Kuhusu malalamiko ya vipimo vya corona kupimwa Dar es Salaam pekee, Ummy alisema wamejipanga na  walishajiandaa kwa jambo hilo na hivi karibuni wataongeza sehemu za kupimia.

“Na hatujazidiwa suala la sampuli kutoka Zanzibar, Kigoma, fuatilieni hata Uganda na Kenya wanafanya hivyo, na sisi tumeanza na moja na tunaongeza zingine na Zanzibar wanaongeza moja.

“Kuna watu wanataka kulifanya hili jambo kuwa la kisiasa, lakini hadi sasa maabara yetu haijazidiwa,” alisema Ummy.

KUONGEZA MAABARA

Pia, alisema maabara za Chuo Kikuu cha Sokoine, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Mbeya, Tanga, Mwanza na Arusha wanaweza kufanya vipimo vya ugonjwa huo kwa sasa.

“Tumeona ipo haja sasa kwa sababu hatuwezi jua tutapata washukiwa wangapi, ila tayari maabara ya Chuo Kikuu cha Sokoine inaweza kufanya vipimo, NIMR Mbeya Tanga, Mwanza na Arusha,” alisema Ummy.

ELIMU KUHUSU UNYANYAPAA

Ummy aliwataka wataalamu wa wizara yake kutoa elimu kwa Watanzania kuhusiana na unyanyapaa kwa wagonjwa ambao watakuwa wamepona.

“Hili nalo linaweza kuwa ni tatizo, hivyo nawaomba wataalamu wa wizara mkatoe elimu, hawa wanaopona wasinyanyapaliwe katika jamii,” alisema Ummy.

WAGENI Z’BAR MWISHO KESHO

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid, alisema wageni kuingia Zanzibar ikifika kesho watawakataza hadi wajue afya za waliowekwa karantini.

“Nchi ni Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, nimezungumzia watu wanaotoka nje ya Tanzania, hata kama ni Mtanzania lakini unatoka nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya siku tatu baki huko huko, tumetoa sababu wengine 134 wapo katika karantini.

“Ikifika Jumamosi tunasema hebu subirini kwanza huko mliko ili tupate nafasi ya kuangalia hawa tulionao, je wapo salama na kwa kiasi gani wameweza kusaidia kupata taarifa za wengine.

“Tumewaambia anayetaka kurudi arudi sasa hivi, lakini hatupangi kufunga mipaka, kama boti yako unataka itembee tu una mafuta yako utembee tu,” alisema Hamad Rashid.

WALIOPO KATANTINI

Hamad Rashid alisema kuna baadhi waliowekwa karantini wamekuwa wasumbufu kwa kudai vyakula ambavyo wanapewa sio wanavyovipenda.

Alisema walitoa maagizo kwamba katika karantini mtu anatakiwa kujilipia mwenyewe na sio kusumbua watu wengine.

“Sasa hivi tunashughulikia waliopo, na waliopo usumbufu ni mkubwa, sijui ‘mimi nimepewa chakula gani?’ Wakati tumewaambia unapokuja unajigharamia mwenyewe, sasa kama kule unaishi peponi kwanini unakuja kuishi motoni?

“Unapotoka huko sisi tumejitahidi, sasa juhudi zetu usizikwamishe, starehe zako fanya wewe,” alisema Hamad Rashid.

MTOTO WA WAZIRI

Waziri huyo alisema mtoto wake alihisiwa kuwa na corona na alikutana na wakati mgumu, lakini anamshukuru Mungu hakukutwa na maambukizi.

“Mtoto wangu alihisiwa na corona tukaenda Muhimbili tukakaa pale, akaulizwa umekutana na watu wangapi akasema si chini ya 50 ikiwemo na mimi.

“Licha ya kuwa ni mwanangu kama ingeonekana kwamba ni positive (ameambukizwa) watu wote 50 ingekuwa positive, hao 50 hatujui na wao wamekutana na wangapi, nataka muone ukubwa wa tatizo na tahadhari ambazo tunachukua.

“Kama hao wakubwa vilemba vimelowa sisi itakuwaje? Nataka hili mlielewe, kama Marekani anapiga kelele, Mfaransa anapiga kelele, wewe masikini usipojipanga itakuwaje?” alisema Hamad Rashid.

MBOWE KARANTINI

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ameshindwa kuhudhuria mazishi ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa (wa kichama) Ilala, Dk. Makongoro Mahanga, baada ya kuwekwa karantini kutokana na mtoto wake Dudley kubainika kuwa na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa salamu za rambirambi za Mbowe zilizosomwa msibani na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema yupo karantini mkoani Dodoma.

“Mimi binafsi nasikitika sitaweza kushiriki kimwili kwenye maziko ya rafiki na mpiganaji mwenzangu. Niko kwenye karantini ya wiki mbili ambapo siwezi kukutana na mtu yeyote hadi itakapothibitika kuwa nami siyo mwathirika.

“Hii ni kwa sababu mwanangu Dudley ni mmojawapo wa wahanga wa kwanza wa janga hili katika nchi yetu. Wataalamu wameishauri familia, nasi tumeafiki kwa moyo mkunjufu, umuhimu wa kufanya “self isolation” hadi hapo itakapothibitishwa kuwa hatujaambukizwa na au hatuwezi kuambukiza wengine.

“Nitashiriki nanyi kwa sala nikiiombea roho ya kamanda wetu pumziko la amani mbinguni. Mpiganaji wetu ametutoka katikati ya janga la dunia. Kwa mila zetu Waafrika, namna mtu ataagwa na kuzikwa siku yake ya mwisho huakisi namna alivyoishi na jamii iliyomzunguka.

“Dk. Mahanga ana kila sifa ya kuagwa na kadamnasi ya watu wa makundi yote, nasi wote tunatamani hivyo, hata hivyo sisi kama wenzake, tuna wajibu kwake wa kuhakikisha kadiri tuwezavyo safari yake ya mwisho isisababishe maafa mengine kwa familia yake ya damu, marafiki na hata familia ya Chadema.

“Nina hakika hata yeye angekuwa hai leo, angeshauri na kukubaliana na tahadhari zinazotolewa, ninaomba wote tuchukue kwa tahadhari kubwa ushiriki wetu kwenye kumuaga mwenzetu. Tujitahidi kadiri tuwezavyo kufuata maelekezo ya namna ya kujikinga na maambukiziya virusi vya corona,” ilisema hotuba yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles