25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitifu ya mfumo wa umeme wa moyo wamepata matibabu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yao ya  moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida  (Tachyarrhythmia’s) wamepata matibabu katika kambi maalum ya matibabu hayo iliyomalizika hivi karibuni  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Kambi hiyo ya siku mbili ilifanywa na madaktari wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mtaalamu mbobezi wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo Dk. Yona Gandye alisema katika hali ya kawaida moyo  hupiga kati ya mapigo 60 hadi 100 kwa dakika.

Wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri wakimtibu mgonjwa mwenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambaye mapigo yake ya  moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida  (Tachyarrhythmia’s) wakati wa kambi maalum siku mbili ya matibabu hayo iliyofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa sita walitibiwa  katika kambi hiyo.

Dk. Gandye alisema mtu akiwa na tatizo katika mfumo wa umeme wa moyo ambalo anaweza kulipata aidha kwa kuzaliwa nalo au athali ya ugonjwa linapelekea mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake inaweza kuwa chini ya mapigo 60  kwa dakika au kuwa juu ya 100 kwa dakika.

“Sababu mbalimbali zinaweza kuufanya moyo udunde kwa haraka kuliko kawaida hii ni pamoja na mtu kuzaliwa  na tatizo, kwa kurithi kutoka  kwa wazazi hata kama wao hawakuwa na dalili. Sababu ya pili ni ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na  kuwa na misuli mikubwa ya moyo (Hypertrophy).

“Mgonjwa anakuja kliniki akiwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi ambazo ni  miguu kuvimba, pumzi kubana, kushindwa kulala vizuri usiku. Ukimfanyia vipimo unakuta moyo wake umetanuka na umefika mahali umeme wake wa moyo haufanyi kazi vizuri,” amesema Dk. Gandye.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo  Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri alisema amefurahi kuona taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefunga mtambo wa kisasa wa Cathlab ambao umeungaishwa na mtambo wa  Carto 3 System 3D &  mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.

Prof. Mervat alisema: “Kufungwa kwa mashine hii ya kisasa na yenye teknlologia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo nchini Tanzania,” amesema.

Alisema katika katika kambi hiyo licha ya kutibu, wataalamu walibadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo unaokwenda kwa haraka.

Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini Misri wanatoa elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu hayo ambapo madaktari wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.

“Hii inamaana kuwa baada ya miaka michache ijayo tutakuwa na madaktari wengi wenye utaalamu wa kutoa matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake  yanakwenda haraka kuliko kawaida  na kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo haya,” alisema Prof. Shams ambaye pia ni mkufunzi katika chuo hicho.

Naye mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Reuben Mutagaiwa ambaye alishiriki  katika kambi hiyo alisema waliandaa wagonjwa ambao walikuwa na  dalili za ugonjwa wa mfumo wa  umeme wa moyo baada ya kuwachunguza kwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Stress Electrocardiography – ECG) waligundulika kuwa na tatizo.

“Ili kuchunguza na kubaini zaidi kuna vipimo ambavyo vinafanyika kwa kitaalamu vinajulikana kama Electrophysiological (EP) studies & ablation ambapo mgonjwa anaingizwa katika  chumba cha upasuaji (Cathlab) kwa ajili ya uchunguzi wa mfumo wa umeme wa moyo (electrophysiology) unasisimua yale matatizo ambayo yalionekana  katika kipimo cha ECG (Induction of Arrhythmias) baada ya kuuleta umeme wa moyo ambao hauna upangilio unaweza kufahamu ni upande gani umeme huo unatoka na kuweza kuudhibiti”, alisema Dkt.Mutagaiwa.

Dk. Mutagaiwa alisema baada ya kugundua kama  tatizo liko kwenye upande wa kushoto au wa kulia wa moyo kuna kifaa maalum kiitwacho  Ablator ambacho kinatoa joto na ukiliweka sehemu ambayo umeme wa moyo hauna mpangilio unatoka unaweza kumtibu mgonjwa kwa kuziunguza njia hizo.

“Kwa kawaida wagonjwa hawa walikuwa wanawekwa katika dawa za vidonge lakini dawa zinaukomo wake, hadi wanafanyiwa matibabu haya walishashindikana kwenye dawa hivyo basi matumizi ya dawa tuliyasimamisha  na kuwafanyia tiba hii,” amesema.

“Faida kubwa ya tiba hii  ni mgonjwa kupona  moja kwa moja na baadaye mgonjwa anashauriwa kutumia dawa na kuendelea na kliniki yake kama kawaida,” alisisitiza Dk. Mutagaiwa.

Matibabu hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika maabara ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (Catheterization Laboratory – Cathlab) mpya ambapo mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kufunga mtambo huo ambao umeungaishwa na mtambo wa  Carto 3 System 3D &  mapping electrophysiology System  wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.

Matibabu ya  tatizo la hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda haraka kuliko kawaida  (Tachyarrhythmia’s) yalianza kutolewa hapa nchini mwaka 2019 ambapo hadi sasa wagonjwa 11 wameshapata matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles