25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa 1530 wapasuliwa moyo Taasisi ya JKCI

Mwandishi wetu, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi, amesema kati ya mwaka 2016-2020, wamefanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 1,537.

Amesema  changamoto kubwa wanayoipata ni wagonjwa wengi kufika katika Taasisi hiyo wakiwa wamechelewa  huku mioyo yao ikiwa imechoka.

Prof Janabi alisema hayo jijini Dar es Salaam juzi baada ya  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Godwin Mollel, alipofanya ziara ya kikazi kwenye taasisi hiyo.

Alisema wagonjwa wanaofika hospitali kwa kuchelewa wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo, wanatumia chupa za damu sita hadi nane lakini kama wangewahi wangeweza kutumia chupa mbili tu za damu.

Prof. Janabi alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuanzisha taasisi hiyo  kwani kabla haijaanzishwa wakati iko kitengo cha magonjwa ya moyo ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa miaka saba (2008 – 2015) walifanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 604 lakini baada ya kuanzishwa kwa JKCI mwaka 2016 hadi sasa  wamefanya  upasuaji kwa wagonjwa 1537.

“Tumefanya upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Grafting-CABG) kwa wagonjwa 100 ambapo asilimia 92 walipona na asilimia nane walipoteza maisha. Tunashukuru tumeokoa maisha ya watanzania ambao hivi sasa wanaendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku”, alisema Prof.Janabi.

View Post

Naye Mkurugenzi  Msaidizi wa huduma za Umma na Binafsi kutoka Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Dk. Vivian Wonanji alisema  wakati ambao nchi yetu inaelekea katika uchumi wa kati idadi ya watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza inaongezeka, hii ni kutokana na mfumo wa maisha ambao watu wanaishi .

“Mwaka jana wizara ilizindua mpango wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufahamu ya magonjwa hayo. Kwa wale ambao wamepata magonjwa hayo yakiwemo magonjwa ya moyo Serikali itahakikisha wanapata huduma za matibabu na ambao hawana magonjwa hayo wanakuwa na uelewa wa kutosha ili waweze kuepuka kupata  magonjwa hayo”, alisema Dk. Wonanji.

Kwa upande wake Dk. Mollel alisema miaka ya nyuma huduma nyingi za kibingwa hazikuwa zinapatikana hapa nchini na hivyo kuifanya Serikali kutumia fedha nyingi kulipia matibabu ya wagonjwa nje ya nchi lakini hivi sasa Serikali imewasomesha wataalamu wa kutosha, imejenga Hospitali za kisasa na kununua vifaa tiba vya kisasa na hivyo  wagonjwa wengi kutibiwa hapa nchini.

“Hivi sasa huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini zimeimarika, kwa upande wa wagonjwa wa moyo wanafanyiwa matibabu ya upasuaji wa kutumia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja na upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na wataalamu wa ndani huduma ambazo hazikuwa zinapatikana hapa nchini,”alisema Dk. Mollel.

Naibu Waziri huyo alisema kazi za kuboresha sekta ya afya zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli zimevuka hadi nje ya nchi ndiyo maana wagonjwa wanakuja kutibiwa hapa nchini  wakitokea  mataifa mbalimbali.

Pia kutokana na madaktari bingwa wabobezi kuwa  wachache  na ili huduma hii  iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi  Serikali imeanzisha program ya tiba mtandao ambayo itawasaidia  wagonjwa walioko mikoani kuweza kupata huduma hukohuko waliko bila ya kufuata huduma hizo Dar es Salaam.

“Kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na janga la ugonjwa corona mipaka ya nchi nyingi ilikuwa imefungwa watu hawakuwa wanasafiri kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, kwa kuwa  Serikali ilikuwa imeboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali huduma zote hizo zilikuwa zinapatikana hapa nchini na wagonjwa walikuwa wanaendelea kutibiwa,” alisema Dk. Mollel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles