27.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Wagombea wanaoumana kumrithi Rais Kabila

Markus Mpangala

MACHO na masikio ya wadau mbalimbali wa kisiasa yanaelekezwa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako wananchi wa Taifa hilo wanatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu.

Awali Tume ya uchaguzi nchini humo, CENI ilitangaza kuwa uchaguzi ungefanyika Desemba 23, mwaka huu, kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu vikiwemo vifaa kutofikishwa vituoni pamoja na ghala za Tume hiyo kuungua moto mjini Kinshasa uchaguzi huo umeahirishwa hadi Desemba 30, mwaka huu.

Takriban wapigakura milioni 46 waliojiandikisha wanatarajia kushiriki zoezi la kuwapigia kura wagombea 34, 900 katika viti 500 vya kitaifa, viti 715 vya mikoa na 21 vya urais na vituo 21,100 vya kupigia kura nchini kote.

CENI ilikuwa na mpango wa kusambaza vifaa vya eletroniki 105,000 kutoka kwa kampuni ya Miru Systems ya nchini Korea kusini. Vifaa vingine vinavyopangwa kutumika ni vile vilivyowahi kutumiwa nchini Ubelgiji, Brazil, India, Namibia na Venezuela.

Hii ni mara ya kwanza mashine za aina hiyo kutumiwa na kuibua wasiwasi kuwa havijafanyiwa majaribio.

Jumla ya wagombea 21 wa urais walioidhinishwa na Tume ya uchaguzi watashiriki katika kinyang’anyiro hicho. Wote wanawania kurithi kiti kinachoachwa wazi na Rais Joseph Kabila ambaye ameliongoza taifa hilo tangu mwaka 2001.

Macho na masikio ya wengi yatatupwa kwa mgombea wa chama tawala cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) Emmanuel Ramazani Shadary.

Tangu awali kulikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuahirishwa na kusogezwa mbele uchaguzi huo miongoni mwa wananchi pamoja na Tume ya uchaguzi (CENI).

Uchaguzi wa DRC umekuwa ukiahirishwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Makala haya yanakupa maelezo mafupi kuhusiana na wagombea wa nafasi za urais mwaka huu nchini humo.

EMMANUEL SHADARY

Ni mzaliwa wa Mji wa Kasongo uliopo Mkoa wa Maniema Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alizaliwa Novemba 29, mwaka 1960. Shadary ni Mkatoliki.

Alipata shahada ya Chuo Kikuu cha Lubumbashi katika masomo ya uongozi na sayansi ya siasa.  Alijiunga katika Chuo Kikuu cha Kinshasa kukamilisha masomo yake ya awamu ya tatu ya sayansi ya siasa na uongozi. Amekuwa akisomea shahada ya udaktari tangu 2015.

Shadary ni baba ya watoto wanane. Amewahi kuwa Naibu na Mkurugenzi Mkuu wa Elimu ya Juu, pamoja na kuwa mwanaharakati wa mashirika ya kijamii mkoani Maniema.

Mwaka 1998 hadi 2001 alikuwa Naibu Gavana wa Jimbo la Maniema chini ya usimamizi wa Rais Laurent Desire Kabila.

Mwaka 2002 alishiriki kuanzisha chama cha PPRD. Tangu mwaka 2005 hadi 2015 alikuwa katibu mkuu anayesimamia masuala ya uchaguzi na nidhamu.

Pia amewahi kuwa mkurugenzi wa kampeni za urais za Joseph Kabila katika Mkoa Maniema.  Aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya PAJ bungeni kati ya mwaka 2006-2011, kabla ya kuchukua uongozi wa chama cha PPRD bungeni mbali na kuwa mshirikishi wa wabunge walio wengi katika Bunge hilo hadi sasa.

Mei 17, 2015, aliteuliwa na Rais Kabila kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha PPRD.

Baada ya Shadary kutangazwa kuwa mrithi wa Rais Kabila, kumezuka minong’ono kuwa si raia halali wa DRC badala yake anaasili ya Kabila la Kitutsi kutoka nchini Rwanda.

Naibu Katibu Mtendaji wa Chama tawala cha PPRD, Ferdinand Kambere, anaamini uteuzi wa Shadary ni alama ya ushujaa wa demokrasia nchini DRC.

FELIX TSHISEKEDI

Felix Tshisekedi ni kiongozi wa Chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) na mgombea wa urais ambaye aliwasilisha fomu yake Agosti 7, mwaka huu.

Ni kiongozi wa chama kikongwe zaidi cha upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tshisekedi aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa pamoja baada ya mazungumzo kati yake na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation), Vital Kamerhe.

Mwafaka kati ya wawili hao uliafikiwa jijini Nairobi Novemba 23, mwaka huu baada ya kushindikana kuwa mgombea wa muungano wa upinzani nchini humo.

Felix Tshisekedi ni mtoto wa mwanzilishi wa chama cha UDPS, mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu Etienne Tshisekedi. Baba yake alifariki Februari mwaka jana, na sasa mtoto wake anatarajia kutumia umaarufu wa mzazi wake kuombea kura za urais.

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55, Novemba 11, mwaka huu akiwa na Vital Kamerhe pamoja na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Martin Fayulu apambane na Shadary. Lakini makubaliano yao yalidumu saa 24 pekee.

Tshisekedi na Kamerhe walidai kushinikizwa na vyama vyao kujiondoa na wakajitenga na Fayulu hatua iliyougawanya upinzani.

Makubaliano yao ni kwamba wakishinda, Tshisekedi atakuwa rais na Kamerhe, ambaye ni rais wa zamani wa Bunge na ambaye aliwania dhidi ya Joseph Kabila mwaka 2011 awe waziri mkuu.

Tangu baba yake alipoanzisha chama cha UDPS mwaka 1982, kilikuwa kama chama kikuu cha upinzani, mwanzoni wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko kisha wakati wa utawala wa Laurent-Desire Kabila, aliyeongoza tangu mwaka 1997 hadi kifo chake 2001.

MARTIN FAYULU

Viongozi wakuu wa upinzani nchini DRC walimpitisha mfanyabiashara maarufu nchini humo Martin Fayulu, kama mgombea wao katika kinyang’anyiro cha uraisi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo.

Fayulu ataingia kwenye uchaguzi huo kutoshana nguvu na mgombea mteule wa serikali, Shadary.

Fayulu mwenye umri wa miaka 61 aliteuliwa baada ya siku kadhaa za mazungumzo baina ya viongozi wakuu wa vyama saba vya upinzani yaliyofanyika mjini Geneva nchini Uswisi.

Mwanasiasa huyo anatoka katika chama cha upinzani cha kinaitwa ACD, na inaarifiwa kuwa mnamo uchaguzi wa mwaka 2011 alimfanyia kampeni kiongozi wa upinzani marehemu Ettiene Tshisekedi.

Fayulu ni miongoni mwa watu wenye ushawishi katika siasa nchini humo. Mbali ya kujihusisha na masuala ya kisiasa ni mfanyabiashara maarufu nchini DRC, miongoni mwa vitega uchumi vyake ni umiliki wa hoteli.

Alisomea nchini Marekani, Ufaransa lakini pia aliwahi kufanya kazi katika kampuni kubwa ya simu nchini Marekani.

Aliwahi kukamatwa mara kadhaa katika maandamano ya upinzani nchini. Wengi wameshangazwa kuchaguliwa kwake, wengi wanamtazama kama mfanyabiashara kuliko kiongozi wa upinzani.

Mgombea huyu anaungwa mkono na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini DRC kama vile Jean Pierre Bemba na Moise Katumbi.

TRYPHON KIN-KIEY MULUMBA

Huyu ni mgombea binafsi. Tryphon Kin-Kiey Mulumba amewahi kuwa msemaji wa rais wa zamani wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko na waziri wa zamani katika Serikali ya Rais Joseph Kabila.

WAGOMBEA WENGINE

Wagombea wengine ni Monique Mukuma, Kikuni Masudi Seth, Mukona Kumbe Kumbe Pierre, Ngoy Ilunga Isidore, Makuta Joseph, Kabamba Noel, Mabaya Jean, Freddy Matungulu,Alain Sekomba, Radjabu Sombolabo, Gabriel Mokia, Basheke Sylvain, Kamerhe Vital, Momba, Charles Gamena, Mbemba Francis.

WALIOKOSA SIFA

Tume ya Uchaguzi CENI iliwaengua wagombea wafuatao baada ya kutokidhi vigezo. Hao ni  Samy Badibanga, Jean-Pierre Bemba, Antoine Gizenga, Marie-Josee Ifoku Mputa, Moise Katumbi, Adolphe Muzito na Bruno Tshibala.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles