Wagombea wanaojitoa, wasiopiga kura wawekwa kwenye lensi ya Takukuru

0
513
Kaimu Mkurugenzi Mkuu (Takukuru), Brigedia Jenerali, John Mbungo

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeahidi kuimarisha mbinu za uchunguzi wa makosa wa rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwamo kutafuta na kupokea taarifa kutoka vyanzo mbalimbali na kuwafikisha mahakamani wanaojihusisha na rushwa.

Pia taasisi hiyo imewataka wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu,wazalendo na wasiojihusisha na vitendo vya rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu (Takukuru), Brigedia Jenerali, John Mbungo, alisema taasisi hiyo imedhamiria kuwaelimisha wananchi waweze kuchagua viongozi ambao wataendeleza yale yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Alisema katika uelimishaji huo wangependa Watanzania wafahamu maana ya uchaguzi lengo lake, sheria za uchaguzi, umuhimu na thamani ya kura yao kuchagua kiongozi bora na asiyejuihusisha na rushwa.

Zaidi alisema wangependa Watanzania umuhimu wa kushirikiana na taasisi hiyo katika kudhibiti rushwa wakati wa uchaguzi.

“Ili kuhakikisha kwamba masuala tajwa yanaelimishwa kwa Watanzania katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, Takukuru imeweka mikakati maalumu ya kufikisha elimu hiyo kwa wananchi wengi kwa kadri iwezekanavyo ili kuhakikisha kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji 2019 unafanyika kwa haki na bila kuwapo kwa vitendo vya rushwa.

“Lengo la kutoa elimu hii ni kuwaandaa wapiga kura pamoja na wagombea kutambua madhara ya rushwa katika kuchagua viongozi ili wawaepuke na pia wawachague viongozi bora wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo katika Taifa letu” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Aliyataja baadhi ya mambo yanayoweza kuhesabika kama rushwa kuwa ni pamoja na mpiga kura kushindwa kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa kuhongwa, mgombea kujitoa kwenye kinyang’anyiro kwa kuhongwa, kutumia njia za rushwa kuandaa kundi au watu kufanya vurugu kwenye mikutano ya kampeni ili mgombea mwingine asipate fursa ya kujinadi kwa wapiga kura.

Mengine ni watu kupewa hongo ili siku ya kupiga kura wasijitokeze, kuamuliwa mtu wa kumpigia kura asiye chaguo lako na kumpa mtu hongo kwa lengo la kumshawishi asitumie vema haki yake ya kupiga kura.

“Pamoja na uelimishaji umma, Takukuru imeshirikisha wadau katika kujadili na kujiwekea mikakati ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi.

“Aprili mwaka huu tulifanya warsha iliyowashirikisha wadau mbalimbali na kujiwekea mikakati ya kila mdau namna atakavyoshiriki katika kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea katika uchaguzi.

“…tuliwaalika wadau kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Msajili wa vyama vya Siasa, Tamisemi, vyombo vya ulinzi na usalama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, idara ya Mahakama, viongozi wa dini, vyombo vya habari na sekta ya bisahara,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here