22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 1, 2022

WAGOMBEA WA UPINZANI WAPUKUTISHWA

Na WAANDISHI WETU,DAR/MIKOANI


WAKATI mchakato wa uchaguzi wa madiwani katika kata mbalimbali nchini ukiendelea, wagombea wa upinzani wengi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo na CUF wamepukutishwa kwa kutupwa nje kwa sababu mbalimbali, ikiwamo uraia na kukosea kujaza fomu.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, jana aliliambia gazeti hili kuwa hadi sasa wagombea udiwani wao 15 katika kata mbalimbali nchini wameenguliwa.

Mrema alisema sasa wako katika hatua ya kukata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema katika kata 78 ambazo ziko wazi, Chadema imesimamisha wagombea kwenye kata 70 na nyingine nane wamewaachia washirika wao katika uchaguzi huo.

“Karibu kila mahali sababu zinafanana, kwa Tarime mgombea mmoja ameenguliwa kwa sababu eti muhuri umepigwa juu ya picha wakati aliyepiga picha ni hakimu na mgombea hahusiki katika hilo zaidi ya hakimu aliyehusika katika kupiga muhuri huo.

“Huko Serengeti wamemwengua mgombea kwa sababu wanadai aliwahi kufungwa, lakini ukweli ni kwamba mgombea aliondolewa kifungo na mahakama na tayari tumeshawasilisha hukumu iliyotolewa na mahakama, lakini tume imekataa kuipokea,” alisema.

Alisema kwa mgombea wa Kimara, Dar es Salaam, tume inadai hakusaini fomu za maadili, lakini ukweli ni kwamba hahusiki na suala la kusaini fomu hizo kwa kuwa tayari uongozi wa juu wa chama ulishazisaini kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 pamoja na vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi na anayesaini ni chama na si mgombea.

Kuhusu wagombea wa Tunduma, alisema NEC inadaiwa kupokea fomu za wagombea ambao Chadema haikuwatuma wala haiwafahamu.

“Chadema haijui kuwa wametokea wapi, kwahiyo msimamizi ndiye anayejua alikowatoa,” alisema.

Alisema katika uchaguzi wa mbunge Jimbo la Buyungu, mgombea wao yuko tayari na anajipanga kuanza kampeni.

ACT WAZALENDO

Katibu wa Kamati ya Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema katika wagombea 20 wa chama hicho waliorejesha fomu, 10 wameondolewa katika kile alichosema ni mazingira yanayoonyesha ni ya makusudi.

Alisema wagombea watatu wameondolewa Tunduma kwa sababu zinazohusu uraia, mmoja Tarime kwa kukosea ujazaji wa fomu, mmoja Kata ya Kimara Ubungo, na wanaendelea kufuatilia taarifa zaidi.

“Tumeshakata rufaa katika ngazi ya wasimamizi wasaidizi kata, lakini tunaendelea kwa ngazi ya wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi katika wilaya na ikishindikana huko tutafika ngazi ya Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.

Mkurugenzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia, hakuweza kutoa ufafanuzi kwa kuwa simu yake iliita muda wote bila kupokewa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa tume hiyo, Emmanuel Kawishe, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa mwenye mamlaka ni mkurugenzi pekee.

HALI ILIVYO

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Msimamizi wa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani, Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Kastory Msigala, alikiri madiwani watano wa CCM wamepita bila kupingwa baada ya wagombea wa Chadema kuondolewa kutokana na kukosa sifa, ikiwamo ya uraia.

Aliwataja waliopita bila kupingwa na kata zao kwenye mabano kuwa ni Franky Mponzi (Majengo), Saimon Mbukwa (Kaloloni), Sogea Julius (Mwavirenga) na Ayubu Mlimba (Mwaka kati) huku akisisitiza kuwa sheria inamruhusu kuwatangaza.

Alisema baadhi ya wagombea waliojitokeza kugombea waliwatilia shaka uraia wao, hivyo kuwasilisha majina yao Ofisi ya Uhamiaji ya Tunduma-Momba kwa uchunguzi zaidi.

“Ni kweli niliwasilisha majina ya baadhi ya wagombea waliojitokeza kugombea nafasi ya udiwani kupitia vyama vya CCM, Chadema na ACT Wazalendo, kuchunguzwa uraia wao na hii inatokana na mazingira ya eneo husika kuwa mpakani na mwingiliano wa watu,” alisema.

Alisema Uhamiaji iliwasilisha majibu ya ombi hilo kwa kuainisha madiwani wanane kwamba si raia wa Tanzania.

Hata hivyo, Msigala alishindwa kuweka wazi majina ya wagombea hao kwa madai kwamba yupo nje ya ofisi, hivyo hawezi kuyataja kwa kufikiri kichwani.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu Dar es Salaam, Ally Mtanda, alisema taarifa za kiuchunguzi juu ya uraia wa madiwani hao wanane, zimewasilishwa kwenye kitengo husika hivyo wanazifanyia kazi na watatolea majibu.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Momba, Twaha Masoud, alisema wanakubaliana na kila uamuzi uliofanywa na NEC.

IRINGA

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, alisema endapo chama hicho kitakufa, basi watumishi wa umma Manispaa ya Iringa na CCM watapata tabu sana.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, alitoa kauli hiyo wakati akizungumzia kasoro na matatizo mbalimbali yanayoendelea katika mchakato wa uchaguzi mdogo unaoendelea Tunduma mkoani Songwe, Wanging’ombe mkoani Njombe na Iringa mjini.

Alisema licha ya kuandika barua za malalamiko kwa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Omary Mkangama na NEC juu ya mwenendo mzima wa ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, lakini hazijajibiwa hata moja.

Msigwa alisema wameshangazwa kuona kwenye mitandao ya kijamii kwamba wagombea udiwani wawili wa kata za Kwakilosa na Ngangilonga wamepita bila ya kupigwa.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Iringa mjini, Mkangama, alikiri kupokea malalamiko ya Chadema, lakini alisema yeye ni msimamizi wa uchaguzi huo.

Alisema anao wasaidizi wake katika kata hizo na ili uchaguzi uweze kwenda vizuri lazima msimamizi msaidizi kwenye kata asimamie hilo.

“Si kweli kwamba nimeshiriki kuhujumu Chadema, michakato yote imefanyika katika ngazi ya kata na kata wamefanya shughuli hizo kwa kuzingatia sheria na kanuni na taratibu pamoja na kanuni zake za uchaguzi za madiwani za 2015,” alisema Mkangama.

 KILIMANJARO

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro, Magreth John, ametuhumiwa na Chadema kuvamia ofisi za Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kelamfua Mokal na kisha kupora fomu za mgombea udiwani wa chama hicho wakati uhakiki wa fomu ukiendelea.

Tuhuma hizo zimeelekezwa kwa msimamizi huyo ikiwa imepita siku moja baada ya mgombea wa udiwani kwa tiketi ya Chadema, Emanuel Vicent Tarimo, kuenguliwa kwenye uchaguzi mdogo katika kata hiyo kutokana madai ya fomu hizo kutokidhi matakwa ya kisheria.

Awali katika barua  yenye kumbukumbu namba HWR/A.50/10VOL11/21 ya Julai 16, mwaka huu iliyoandikwa na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, kwa mgombea huyo wa udiwani,  ilimtaarifu kutoteuliwa kugombea nafasi hiyo baada ya fomu zake nne  alizojaza  kuwa na makosa mbalimbali.

Kwa habari kamili jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA hapo juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,373FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles