30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea urais wachuana mdahalo wa Twaweza

annelyimochiefrungwe hashimNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

WAGOMBEA urais wa vyama vya ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chifu Lutasola Yemba, Chama Cha Ukombozi  wa Umma (CHAUMA), Hashimu Rungwe na Chama cha Tanzania Labor (TLP), Macmillan Lyimo wamechuana katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza.

Mdahalo huo uliofanyika Dar es Salaam jana uliwashirikisha wagombea hao huku mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawakushiriki kutokana na dharura za kampeni zao zinazoendelea mikoani.

Katika mdahalo huo, wagombea hao walikuwa na kazi ya kujibu maswali mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Taifa yaliulizwa moja kwa moja kutoka kwa washiriki na mengine ya mitandaoni.

Baadhi ya mambo walioyafafanua wagombea hao ilikuwa ni sababu za wao kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya urais.

Akielezea sababu za uamuzi wake wa kuwania nafasi hiyo, Mghwira, alisema ana uwezo wa kushika nafasi hiyo kwa sababu kitaaluma ni mwanasheria na amefanikiwa kusoma masomo ya theolojia inayomuwezesha kuongoza watu.

Akizungumzia uamuzi wake wa kuwania nafasi hiyo, Yemba, alisema unatokana na elimu yake ya miamba na uwezo wake wa kusimamia haki sawa kwa kila mwananchi bila ya kubagua.

Wakizungumzia kuhusu ufisadi na rushwa, Mghwira, alisema atahakikisha anasimamia uboreshaji wa maslahi kwa taasisi za Jeshi la Polisi, mahakama na walimu na kuingiza katika mitaala ya elimu kuanzia shule ya awali hadi vyuo vikuu.

Alisema watahakikisha wanakusanya mapato ya kutosha ikiwamo udhibiti wa ukusanyaji wa kodi ili waweze kutoa usawa kwa watu wote na kuwawezesha kupata huduma za jamii sawa.

Akijibu swali la kutaka kujua tofauti ya mtawala na kiongozi, Yemba, alisema mtawala ni mtu anayechukua rasilimali za wengi na kuwanufaisha wachache wakati uongozi ni ushirikishwaji wa watu wote katika kunufaika na rasilimali za taifa.

Naye Mghwira, alisema mtawala ni mtu anayetoa amri au maagizo anayohitaji kutekelezwa bila ya kujali kama anaowaongoza wanapenda au hawapendi, wakati kiongozi ni mtu anayewajibika kwa wananchi na kutoa mrejesho kwao.

Kuhusu suala la uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema imekuwa ikijitahidi kwa kiwango fulani lakini si huru kutokana na kuingiliwa na viongozi wakuu wa nchi.

Akizungumzia Katiba anayoiamini, Yemba, alisema ni ile iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba na kama akipewa nafasi atahakikisha anairejesha tena kwa wananchi ili kuifanyia marekebisho na kuwa na maoni ya watu wengi.

Wakizungumzia kuhusu suala la ukuzaji wa uchumi na viwanda, Mghwira, alisema atahakikisha anawashirikisha wananchi kuweka miundombinu.

Kwa upande wake, Lyimo, aliyefika akiwa amechelewa alizungumzia suala la huduma ya afya na kusema chama chake kikiingia madarakani watatoa huduma za afya bila ya kuwepo kwa matabaka.

Naye Mghwira alisema ilani yao inawataka kutoa huduma ya afya bure kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma hiyo kupitia mifuko ya jamii itakayowawezesha kupata mikopo.

Kuhusu suala la huduma ya afya, Yemba, alisema chama chake kinaamini wajibu wa kuwatibu wagonjwa utakuwa juu ya Serikali.

Akizungumzia kuhusu suala la amani, Rungwe, aliyechelewa katika mdahalo huo na kukuta hoja ya mwisho alisema ni ngumu kulinda amani katika nchi ambayo watu wake wana njaa kila mahali.

Alisema akipata nafasi hiyo atahakikisha anaondoa njaa kwa wananchi wote ili amani iweze kuendelea kutamalaki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles