25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea urais CCM wavurugwa

Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

KATIKA kile kinachoonekana ni kuvuruga kambi za wagombea urais mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepangua makatibu wa mikoa 17 kwa kuwahamisha vituo vyao vya kazi.

Makatibu hao ni pamoja na Mary Chatanda aliyekuwa Mkoa wa Arusha, ambaye kwa sasa amehamishiwa Singida.

Chatanda kwa muda mrefu amekuwa na msuguano ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, huku kiini chake kikidaiwa ni misimamo tofauti ya vijana hao kumuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa watakaoomba kugombea urais kupitia chama hicho mwakani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa ndani na nje ya chama hicho tawala, wanaona hatua ya kupangua idadi kubwa ya watendaji wa mikoa huku kukiwa kumebakia miezi michache kinyang’anyiro cha kugombea kuwania urais kuanza mwakani, inalenga kuvunja mitandao ya urais au njia ya kujipanga na uchaguzi mkuu.

“Kuna mambo mawili makubwa, CCM ama inavunja mitandao ya urais iliyojengwa na watendaji hawa, au inajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwakani,” alisema kada mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Alisema panguapangua hii ya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, ambaye anachukuliwa kama mtu muhimu ndani ya chama hicho katika kushinda chaguzi mbalimbali, inaweza ikawa imebeba siri kubwa.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba CMM/OKM/M.11/Vol.7/1, yenye kichwa cha habari “Uhamisho wa Makatibu wa Mikoa” iliyosainiwa na Kinana Septemba Mosi, Alphonce Kayanda, amehamishwa kutoka Mkoa wa Katavi kwenda Arusha.

Barua hiyo, inaonyesha kuwa Joyce Kasunga amehamishwa kutoka Mwanza kwenda Pwani,na  Janeth Kayanda anatoka Bukoba Mjini kwenda Tabora.

Kinana aliwataja wengine ni Gustav Muba anayehamia Geita kutoka Tanga, Sauda Mpambalyoto anayekwenda Kusini Unguja akitokea Pwani na Evelyine Mushi anayetoka Kagera kwenda Katavi.

Makatibu wengine wanaohamishwa vituo vyao vya kazi ni Naomi Kapambala anayetoka Singida kwenda Kigoma, Idd Ame kutoka Tabora kwenda Kagera na Shija Othman Shija ambaye anatoka Kusini Pemba anakwenda Tanga.

Uhamisho umewagusa pia Mwangi R. Kundya kutoka Mjini Magharibi kwenda Mbeya, Mohamed Nyawenga anatoka Kigoma kwenda Mjini Mangaribi, Adam Ngalawa anatoka Shinyanga kwenda Mara na Maganga Sengelema anatoka Mbeya kwenda Shinyanga.

Wengine ni Zainab Shomari anayetoka Kusini Unguja ambaye kwa mujibu wa barua hiyo amepewa likizo miezi miwili, Mary Maziku anatoka Geita anakwenda Makao Makuu Dodoma na Bernad Nduta anatoka Makao Makuu anakwenda Mwanza.

Kutokana na uhamisho huo na hasa kwa Katibu wa CCM Arusha, Chatanda, MTANZANIA lilitafuta maoni ya wadau wa siasa ili kujua wanazungumziaje kuhusu uhamisho wake.

Kwa upande wake, Kada wa CCM mkoani Arusha ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini, aliliambia MTANZANIA kwamba uhamisho huo ni wa kawaida wa kikazi.

“Siasa ni mchezo wa makundi, hivyo siamini kama kuondoka kwake vurugu zilizokuwa ndani ya CCM hapa Arusha zitaisha. Tofauti lazima ziendelee.

“Lakini kwa upande mwingine naamini itatuletea amani kwa CCM hapa Arusha japo hatujui anayekuja ana tabia zipi na, kwani inaweza ikawa afadhali anayeondoka kuliko ajaye,” alisema kada huyo.

Tangu Chatanda ahamishiwe Arusha hali ya kisiasa mkoani humo imekuwa ni ya vuta nikuvute baina ya CCM na vyama vya upinzani na wakati mwingine ndani ya chama hicho tawala.

Juhudi za MTANZANIA kupata ufafanuzi wa viongozi wa juu wa CCM kuhusu uhamisho huo ziligonga mwamba hadi tunakwenda mitamboni baada ya simu ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Philip Mangula simu yake kuita na kukatwa huku ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ikiita bila kupokelewa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. DUUUU Hii nzuri kama uhamisho una hela watapata hela ya uhamisho maisha yatasonga.huku ni kujipanga kwa uchaguzi au kukomoana.wapeni makati wa wilya kaziya mkoa kama MAMA WA WILAYA YA KARAMBO(SUMBAWANGA)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles