27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga wakuu watakiwa kutoa elimu ya corona

Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anayesimamia Idara Kuu ya Afya, Dk. Zainab Chaula, amesema wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoletwa na virusi vya corona (Covid-19) ili kuepusha usisambae endapo atatokea mtu mwenye virusi hivyo.

Alisema hayo wakati wa mkutano wa taifa wa waganga wakuu wa mikoa (RMOs) wa kujadili utayari, changamoto na hatua za kukabiliana na tishio la virusi hivyo uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila. 

“Katika mkoa wewe mganga mkuu ndio mtaalamu namba moja wa afya kwenye mkoa wako ambalo ndilo eneo lako la kazi, mnatakiwa kushauri viongozi katika kukabiliana na ugonjwa huu,” alisema Dk. Chaula. 

Alisema upashanaji elimu kuhusu kujikinga na maambukizi kwa wananchi ni jambo muhimu kwani jamii inapaswa kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya ugonjwa huo unavyoambukizwa na dalili zake ili kila rika liweze kuwa na ufahamu na hivyo itasaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini. 

“Kama nchi za Afrika hivi sasa hatupo kwenye hatua ya utayari bali kwenye hatua ya kukabiliana. Kwani utaona ugonjwa huu umezikumba nchi nyingine, kama nchi lazima wataalamu wote tujiandae kukabiliana na virusi hivi vya corona ili endapo tutapata mgonjwa, basi vyanzo vyote vya maambukizi vinatakiwa kudhibitiwa ili usienee,” alisema Dk. Chaula. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tamisemi anayeshughulikia afya, Dk. Doroth Gwajima alisema ofisi yake wapo tayari kupokea maelekezo na mafunzo yote ya kisekta ili kutimiza lengo tarajiwa la Serikali la kudhibiti na kukabiliana na ugonjwa huo. 

Dk. Gwajima alisema mkutano huu utasaidia waganga wakuu wa mikoa nchini kutoka na mkakati wa pamoja wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu, hususan mikoa ya mipakani kama Kagera, Katavi, Songwe, Kigoma pamoja na mikoa mingine ambayo ipo kwenye hatari ya kuingia kwa magonjwa ya mlipuko. 

Hata hivyo, aliwataka waganga wakuu hao kutoa mafunzo kwa wataalamu wengine wa chini yao na viongozi wa mikoa na halmashauri ili kwenda pamoja katika kukabiliana na magonjwa wakati wa dharura. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles