27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAFUGAJI WAOMBA KUINGIZA MIFUGO HIFADHI ZA TAIFA

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha wafugaji Tanzania (CWT), kimeiomba Serikali kuwaruhusu kuingiza mifugo yao katika hifadhi za taifa kwa dharura ili kuinusuru kutokana na ukame unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Wafugaji hao walisema hali ya ukame imekuwa tishio na tayari wamepoteza mifugo mingi inayokufa kwa njaa baada ya majani kukauka kutokana na kukosa mvua kwa muda mrefu.

Sambamba na hilo, pia wamealaani matukio ya kuuawa kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini, likiwamo lililotokea hivi karibuni wilayani Arumeru mkoani Arusha ambako watu wanne wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kudaiwa kupigwa risasi za moto na askari wa Suma JKT.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa CWT, Magembe Makoye, alisema Serikali ilichukulie suala la ukame kuwa ni dharura na hivyo iwaruhusu kuingiza mifugo ili kupata chakula katika hifadhi hizo na baada ya ukame kupungua mifugo hiyo irudishwe maeneo yake ya awali.

“Tunaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na ile ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuangalia namna ya kuwasaidia wafugaji ili kunusuru mifugo yao ambayo ndiyo uchumi wao na taifa kwa ujumla.

“Katika hili, tunashauri wafugaji waruhusiwe kuingiza mifugo hiyo japo mara mbili kwa wiki, wakati wakisubiri mvua kunyesha,” alisema Makoye.

Kuhusu mauaji, Makoye alisema kuwa ni ya ukandamizaji dhidi ya wafugaji.

“Upo utaratibu wa kisheria wa kuwaondoa wafugaji katika maeneo yasiyo rasmi, lakini si kwa kuwapiga risasi na kuwaua,” alisema Makoye.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Francis Nzuki, alisema kuwaua wafugaji na hata makundi mengine ni uvunjifu wa haki za binadamu jambo ambalo hawatalifumbia macho.

Katika hatua nyingine, Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umeikumbusha Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwapatia wananchi Katiba mpya kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa haki za binadamu uliofanyika Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo uliohusisha pia asasi za kiraia na THBUB, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengulumwa, alisema Tanzania iliridhia mapendekezo 133, likiwamo la kutengeneza Katiba mpya ya wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles