Na Derick Milton, Meatu
WAFUGAJI wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, wanaoishi mpakani mwa pori la akiba la Maswa na Hifadhi ya Taifa Serengeti wameeleza tatizo linalotesa mifugo yao hasa ng’ombe ni kushambuliwa na magonjwa mengi ya ajabu ikiwamo kuvimba, kupasuka miguu na kufa.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa huo, David Kafulila wakati wa kikao chake na wafugaji hao jana katika ukumbi wa Halmashuari ya wilaya hiyo, wamesema kuwa magonjwa hayo yamesababisha ng’ombe wengi kufa, kuvimba mwili mzima, kupasuka kwato, kuvimba mapafu pamoja na kutoa udenda
Wameiomba serikali kuwasaidia upatikanaji wa chanjo ya haraka ili kinusuru mifugo yao.
“Nilikuwa na ng’ombe 80 lakini mpaka sasa nimebaki na ng’ombe 37 tu, wengine wote wamekufa kutokana na magonjwa hayo, tunaomba sisi wafugaji hasa tunaopakana na hifadhi serikali itusaidie,” amesema mfugaji Shoka Felesi.
Naye Hunge hunge amesema pamoja na magonjwa, changamoto nyingine ni ukosefu wa majosho na malambo ya kunyweshea mifugo yao, hivyo wameiomba serikali kuwatatulia kero hizo.
“Tunayo shida kubwa ya ukosefu wa majosho, ndiyo maana mifugo yetu inapata magonjwa mara kwa mara, hatuna majosho, lakini hata chanjo hatupati kwa muda mrefu,” amesema Hunge.
Kwa upande wake Ofisa Mifugo wa Halmashauri hiyo, Hussen Nyenye, amekiri kuwepo kwa magonjwa hayo, ambayo alieleza yanasababishwa na mwingiliano uiliopo kati ya mifugo na wanyama kutoka hifadhini.
“Tatizo ni wafugaji wetu wengi kupeleka mifugo yao kwenye hifadhi ndiyo maana wanapata magonjwa mbalimbali, lakini tumekuwa tukitoa chanjo ila wanaojitokeza wachache na kwa mwaka huu bado hatujatoa chanjo,” amesema Nyenye.
Naye Mkuu wa Mkoa amemtaka mkurugenzi wa halmashuari hiyo kumpatia taarifa ya tahadhari inayotokana na magonjwa hayo ili kujua ukubwa wa tatizo ili aweze kuwaombea msaada kutoka wizarani.
“Waziri wa mifugo anatoka mkoa wa Simiyu, leo nitamweleza tatizo hili ili kuona wanaweza kutusaidia vipi kwa haraka kutatua shida hii, lakini nipate taarifa ya ukubwa wa tatizo hili,” amesema Kafulila.
Katika kikao hicho wakulima waliiomba serikali kuanzisha mkakati wa upandaji wa nyasi za kisasa ili kuweza kukabiliana na changamoto ya malisho ikiwa pamoja na kupatiwa elimu ya ufugaji wa kisasa.
Wafugaji hao wamesema wako tayari kupata mbengu hizo kwani wameona suluhisho la malisho si kuongezewa maeneo, bali ni kufuga kisasa ikiwemo kupanda nyasi.