23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wafuasi wa Ruto wadai Uhuru atamtema Raila

NAIROBI, KENYA

MWAFAKA baina ya Rais Uhuru Kenyatta na mwanasiasa wa upinzani, Raila Odinga umeendelea kuzua hasira miongoni mwa wanasiasa wa Chama cha Jubilee, huku baadhi yao wakidai kiongozi huyo wa ODM atatemwa uchaguzi wa 2022 utakapokaribia.

Katika eneo la Mlima Kenya, wabunge wa Jubilee walitofautiana iwapo mwafaka huo maarufu kama ‘Handshake’ unalenga kusambaratisha ndoto ya Naibu Rais William Ruto kutaka kuwa rais.

Mbunge wa Mukurweini, Anthony Kiai alimtaka Rais Uhuru kuachana na Odinga ili kunusuru ndoto ya Dk. Ruto kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, Kiai alidai kuna dalili Rais Uhuru atamkwepa Odinga kabla ya uchaguzi mkuu na kumuunga mkono Dk. Ruto.

Kiai alisema mgawanyiko unaoshuhudiwa ndani ya Jubilee kwa sasa umesababishwa na mwafaka huo wa kushikana mikono baina ya Rais Uhuru na Odinga.

“Chama cha Jubilee tayari kimegawanyika, na tunamtaka Rais Uhuru kufutilia mbali ‘Handshake’ ili kunusuru chama,” alisema Kiai.

Mbunge wa Ndaragwa, Jeremiah Kioni, hata hivyo, alitofautiana naye, akisema ‘Handshake’ inafaa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alisema kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Dk. Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Katika eneo la Kati, tunajali sana urafiki kwani Dk. Ruto amekuwa rafiki yetu tangu mwaka 2012. Tuna imani atashinda vikwazo vyote ambavyo amewekewa na atakuwa Rais 2022,” alisema  Gachagua.

Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa alishutumu kundi la Kieleweke linalompinga Dk. Ruto kuwa linalenga kuzua vurugu ndani ya Jubilee ili kupata mwanya wa kujiunga na vyama vingine.

Wabunge Githinji Gichimu (Gichugu) na Samuel Gachobe (Subukia), hata hivyo walisisitiza kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya Jubilee.

Wawili hao walisema kuna baadhi ya wanasiasa walio tatizo ambao hawakuwataja, waliogawanyika ndani ya Jubilee katika makundi mawili; TangaTanga na Kieweleke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles