na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
KIKUNDI cha wafanyakazi wa kike wanaofanya kazi katika kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML ladies) wanaofanya kazi mjini Geita, wametoa msaada wa vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia kina mama wajawazito na wazazi wanaojifungua katika hospitali ya Nzela na kituo cha Afya Kasota zilizopo katika halmashauri ya Wilaya Geita.
Akizungumzia msaada huo uliotolewa jana Mjini Geita, Makamu mwenyekiti wa kikundi hicho, Lina Sitta alisema wanawake wanaofanya kazi GGML wameguswa na changamoto za uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya katika vijiji vinavyowazunguka.
“Tumeona kwa sasa tuanze na vijiji vya Kasota na Nzela ambavyo vipo karibu zaidi na mgodi wa GGML na tumekuwa tukiona changamoto ya akina mama kukosa sabuni,taulo za mama waliojifungua na nepi za watoto.Msaada huu tumeutoa maalum kuadhimisha siku ya wanawake duniani,” alisema.
Mganga Msaidizi wa kituo cha afya Kasota, Stanley Victor amewashukuru GGML ladies kwa kutoa msaada huo lakini pia kwa GGML kusaidia ujenzi wa maabara, nyumba ya mtumishi na jengo la baba na mtoto kituoni hapo.
“Mmeitendea haki siku ya wanawake duniani mwaka huu.Wagonjwa wengi waliopo hapa wamefarijika sana kutokana na msaada huu,”alisema.
Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani mwaka huu ni Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia: chachu katika kuleta usawa wa kijinsia.