Na Tiganya Vincent, Maelezo-TABORA
KATIBU Tawala Mkoa wa Tabora, Dk. Thea Ntara amemtaka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete kuwakamata na kuwafikisha polisi watumishi wawili wa hospitali hiyo wanaotuhumiwa kukutwa na dawa na vifaa tiba katika mikoba yao.
Kauli hiyo aliitoa jana   baada ya watumishi hao kukamatwa na vifaa hivyo ambavyo ni  dawa   na vifaa vya hospitali wakitaka kwenda kuviuza katika hospitali binafsi.
Alisema     dawa na vifaa tiba hivyo havitakiwi kutoka nje ya hospitali na havikuwa na maelekezo ya mganga.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwapongeza walinzi waliofanya kazi hiyo na kuwaagiza kuongeza kupekua watu wote wanaokwenda kuona wagonjwa kwa sababu inawezekana watumishi wengine ambao siyo waadilifu wakatumia fursa hiyo kutorosha dawa na vifaa tiba vingine.
Vifaa na dawa vilivyokamatwa ni Cannula, Surgical gloves, Syringesa, Urinal bag, IV giving set, Blood giving set, Brainded silk number, water injection, powder, soap, examination glove, gentamyacin injection ampule, ascorbic acid.
Hospitali hiyo imekuwa ikikumbana na wizi wa mara kwa mara hatua iliyosababisha  Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuisimamisha kampuni iliyokuwa imepewa jukumu la kulinda.
Ofisi hiyo iliweka kampuni nyingine wakati taratibu za kuichukulia hatua kampuni ya awali zikiendelea.