30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

WAFANYAKAZI SERENA WADAI KUNYANYASWA

Safina Sarwatt, Arusha

Wafanyakazi wa Hoteli ya Kitalii, Serena Resort iliyopo nje kidogo ya Jiji la Arusha, wameitaka Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira kuitupia macho hoteli hiyo kwa madai ya kukithiri kwa unyanyasaji kutoka kwa uongozi wa hoteli hiyo.

Aidha, wamedai wamekuwa wakitishiwa kufukuzwa kazi pindi wanapodai kuboreshewa mazingira ya kazi hatua amabayo imewafanya baadhi yao kukaa kimya kwa hofu ya kufukuzwa kazi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, wafanyakazi hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe kwa sababu za kiusalama, wamedai kwa muda mrefu uongozi wa hoteli hiyo umekuwa ukiwanyanyasa huku madai yao yakipuuzwa na wakati huo huo wafanyakazi kutoka nchini Kenya wakipewa huduma nzuri ikiwamo mishahara minono na maslahi mengine.

Baadhi ya mambo wanayolalamikia wafanyakazi hao ni kutopatiwa huduma ya matibabu kutokana na mwajiri wao kufuta huduma ya matibabu kupitia Bima ya Afya (NHIF), huku wakitibiwa kupitia Bima ya Jubilee ambayo haiwapi nafasi ya kwenda kutibiwa katika hospitali za rufaa.

“Changamoto nyingine hatupewi posho ya usafiri wa kutoka nyumbani kwenda kazini na kurudi nyumbani hali inayotulazimu kutumia zaidi ya Sh 10,000 kwa siku kama gharama za usafiri.

“Tunaomba mtusaidie kwa kweli hali ni mbaya, wafanyakazi wa Kitanzania tunanyanyasika sana tofauti na wenzetu wa Kenya ambao wanaishi vizuri licha ya baadhi yao kutokuwa na uwezo ya kufanya kazi ambazo tuna uwezo nazo,” amesema mmoja wa wafanyakazi hao.

Hata hivyo, Meneja Rasilimali Watu wa hoteli hiyo, John Mwamakula amekana tuhuma hizo akidai ofisi yake hajawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wafanyakazi hao wakilalamikia manyanyaso na kwamba ina utaratibu wa wafanyakazi kuwasilisha malalamiko yao ikiwamo utoaji taarifa kwa njia ya siri.

Lakini pamoja na licha ya kudai kutokupokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao, meneja huyo amekiri wafanyakazi hao kuondolewa asilimia tano ya mshahara wao kwa kile alichodai ni kuyumba kwa biashara ya utalii mwaka jana.

“Biashara ya utalii iliyumba sana mwaka jana ndiyo maana tukaondoa asilimia tano ya mshahara kwa makubaliano kwamba Juni mwaka huu tutakaa tena kuangalia mkataba kwa lengo la kuuboresha na kuongeza mshahara,” amesema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles