31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi OBC wakiri, watakiwa kulipa mil 100/-

Janeth Mushi- Arusha

MAHAKAMA ya Wilaya ya Arusha imewatia hatiani raia 10 wa kigeni, waliokuwa wakifanya kazi bila vibali hapa nchini na kuwatoza faini ya Sh milioni 100 au kutumikia kifungo cha miezi 12 jela kila mmoja.

Hatua hiyo imekuja jana baada ya watuhumiwa hao ambao walikuwa wakifanya kazi katika Kampuni ya wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu ya Otterlo Business Cooperation (OBC), iliyopo eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro, mkoani hapa ikijishughulisha na shughuli za uwindaji wa kitalii, kukiri makosa yanayowakabili.

Mbali na raia hao wa kigeni, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Isack Mollel, ambaye hakuwa tayari kukiri mashtaka 37 ya kujishughulisha na kuajiri raia hao bila kuwa na vibali halali vya kufanya kazi nchini wala cheti cha msamaha, kinyume na sheria ya kuratibu ajira na mahusiano ya wageni.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Rose Ngoka, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Mkuu Martenus Marandu, Wakili Mwandamizi Abdallah Chavula na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Idara ya Kazi, Emanuel Mweta.

Washitakiwa hao ni Darweshi Jumma, Riaz Aziz Khan, Mohammad Tayyab, Ali Bakhsh, Abdul Ahman Muhammad, Martin Crasta, Imtiazd Fiaz, Arshad Muhammad, Hamza Sharif na Zukfiqar Ali ambao walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali ikiwemo ufundi magari, wapishi, madereva na wapaka rangi nyumba.

Washtakiwa hao waliwakilishwa na Wakili Steven Mosha huku Mollel akiwakilishwa na Wakili Goodluck Peter.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ngoka alisema baada ya kuzingatia maombi yaliyotolewa na Wakili Mosha na kwa kuangalia mazingira ya kesi hiyo, mahakama hiyo inawataka kuwa waangalifu kwa kutii sheria, kanuni na taratibu za nchi hii na kuwatoza kila mmoja faini ya Sh milioni 10 au kifungo miezi 12 kila mmoja.

“Mahakama hii inawatia hatiani mshtakiwa wa pili hadi wa 11 kwa kukiri wenyewe makosa ya kujihusisha na ajira wakati siyo raia wa Tanzania.

 “Mahakama inaamuru kila mshtakiwa kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, kila mmoja alipe faini ya Sh milioni 10 au wakishindwa kila mmoja atumikie kifungo cha miezi 12. Haki ya kukata rufaa ipo kwa ambaye hajaridhika na uamuzi,” alisema.

Awali Wakili Marandu alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa washitakiwa kukumbushwa mashtaka yao.

Kwa mujibu wa barua waliyoandika na kusaini kupitia wakili wao (Mosha), washtakiwa hao isipokuwa Mollel, walieleza nia yao ya kutaka kukiri kosa, ndiyo maana Jamhuri iliamua kupeleka kesi hiyo mahakamani ili waeleze nia yao.

“Jamhuri tupo tayari kuendelea kwa kuwakumbusha mashtaka yao kuanzia kosa la 38 hadi 47, kwani shtaka la kwanza hadi la 37 yanamhusu Mollel ambaye hayuko tayari kukiri kama alivyoeleza wakili wake (Peter),” alidai Marandu.

Kupitia mkalimani wao Mohamed Abas ambaye alikuwa akiwatafsiria kwa lugha ya Kihindi, Wakili Mweta aliwakumbusha washtakiwa hao makosa yao, na walikiri kufanya kazi nchini bila vibali kati ya Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Baada ya watuhumiwa hao kusomewa maelezo hayo ya awali, Wakili Marandu aliomba mahakama hiyo kutoa adhabu inayowastahili na kuwa hakuna kumbukumbu ya makosa kama hayo kwa washtakiwa hao.

“Mheshimiwa hakimu nina maombolezo kadhaa ikiwemo watuhumiwa kutokuwa na rekodi ya makosa kama haya, tunaomba wapewe adhabu ndogo kutokana na utayari wao wa kukiri na kukubali makosa yao, hivyo wameipunguzia mahakama muda,” alisema.

Washtakiwa wote 10 waliachiwa baada ya kulipa faini hiyo.

Awali Septemba 2 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliwaachia huru watuhumiwa hao baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasomea maelezo ya awali kwa zaidi ya mara nne, lakini walikamatwa tena na polisi na kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Arusha.

Kutokana na Mollel kutokukiri mashtaka yanayomkabili, kesi yake ilipangwa kutajwa Oktoba 16.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles