23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

WAFANYAKAZI KENYA WAPEWA NYONGEZA YA ASILIMIA TANO

NAIROBI, KENYA


RAIS Uhuru Kenyatta, ametangaza nyongeza ya asilimia tano kwa kiwango cha chini cha mshahara nchini Kenya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi.

Tangazo hilo lilitolewa jana kwa niaba yake na Waziri wa Kazi, Balozi Ukur Yatani Kanacho aliyewaongoza viongozi wengine mashuhuri serikalini na upinzani kuadhimisha siku hiyo kwenye Viwanja vya Uhuru Park, jijini Nairobi.

“Wafanyakazi wa umma watapata nyongeza ya asilimia tano,” alisema Rais Kenyatta kwenye hotuba yake iliyosomwa na Waziri Yatani.

Hotuba ya Kenyatta iliegemea nguzo zake kuu nne katika awamu yake ya pili na ya mwisho ambazo ni; kuangazia usalama wa chakula, makazi bora na nafuu, ujenzi wa viwanda ili kukabiliana na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, na matibabu bora.

Kenyatta mwaka 2017 alitangaza nyongeza ya asilimia 18 kwa wafanyakazi wa umma.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa wafanyakazi (Cotu), Francis Atwoli amesema agizo hilo halijatekelezwa kwa baadhi ya kampuni na taasisi.

“Kuna kampuni nyingi hazijatekeleza agizo hilo. Rais pia alipendekeza kodi kwa wanaopokea mshahara wa chini ya Sh100,000 upunguzwe lakini hayo yote hayajaheshimiwa,” alisema Atwoli.

Cotu pia imekosoa pendekezo linaloongozwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale la kutathmini sheria za kudhibiti miungano ya wafanyakazi kwa lengo la kupunguza majukumu yao.

Miungano ya wafanyakazi Kenya imekuwa ikiandaa migomo ya kitaifa, ili kutetea haki zao na mbunge huyo wa Garissa mjini anapania kuwasilisha muswada bungeni wa kudhibiti miungano hiyo.

“Waziri Ukur Yattani tunakushauri ujiondoe kwa mjadala huo wa kurekebisha sheria za miungano ya wafanyakazi,” Atwoli alionya.

Kinara wa upinzani Raila Odinga aliyehudhuria maadhimisho hayo, alisema makubaliano yake na Rais Uhuru Kenyatta ya Machi 2018, yalilenga kuimarisha maisha ya Wakenya.

“Mazungumzo yetu yaliegemea kuimarisha maisha ya wananchi wote, kwa msingi wa bidhaa na kodi nafuu ya nyumba,” alisema Odinga.

Aliongeza kuwa Nasa imeungana na Serikali ya Jubilee ili kuangazia masaibu yanayokumba Wakenya ikiwamo kukabiliana na kero za ufisadi.

Kadhalika, kiongozi huyo alizingumzia kuhusu marufuku ya Nasa kununua bidhaa za kampuni zilizounga utawala wa Jubilee, akisema kutokana na makubaliano yake na Kenyatta wamezisamehe na hivyo wafuasi wake waache kuzisusia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,303FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles