25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi hewa jinamizi la Nigeria ndani ya Tanzania

President-Muhammadu-BuhariNa Aloyce Ndeleio

KWENYE makala  moja iliyobeba kichwa cha habari “Kwa ukwapuaji  hautofautiani na Nigeria” kwenye Gazeti hili Januari 27 mwaka huu, nilifahamisha namna ambavyo maofisa waandamizi wa Serikali ya nchi hiyo walivyokuwa wamekwapua  mabilioni ya fedha kutoka kwenye mabenki ya nchi hiyo.

Hali hiyo haikutofautiana na hali ya ukwepaji kodi uliofanywa na baadhi ya watu kwenye Serikali  nchini Tanzania na jinsi walivyokwapua mabilioni ya fedha  kutoka Benki Kuu mambo yaliyoibua kashfa kadhaa na hata kusababisha baadhi ya maofisa hao kujiuzulu.

Wakati nchini Nigeria unaweza kusikia kuwa lori la mafuta limeibwa  na lisionekana licha ya kwamba lilipita kwenye barabara  ndani ya miji ya nchi hiyo kwa Tanzania  unaweza kusikia kontena  lilipita  kwenye Bandari ya Dar es Salaam kimya kimya na si mtoza kodi wala ushuru aliyeliona.

Pamoja na hali hiyo  suala jingine  ambalo linaonesha kuwa kila linalotokea Nigeria mwangwi wake hupokelewa na Tanzania ni hili kadhia ya kuwapo kwa wafanyakazi hewa kwenye ofisi za umma na hivyo kuifanya Serikali kupoteza  fedha nyingi. Hivyo  Taasisi ya Kupambana na Rushwa nchini Nigeria imebaini kuwapo kwa wafanyakazi hewa 37,000 kwenye orodha ya malipo  ya wafanyakazi serikalini  na kwamba  idadi hiyo bado itaongezeka.

Kaimu mwenyekiti wa Taasisi hiyo inayojulikana kama Tume ya  Uchumi na Uhalifu wa Kifedha (EFCC), Ibrahim Magu alisema kuwa maelfu ya wafanyakazi ambao hawapo kwenye orodha ya wafanyakazi serikalini imeigharimu Serikali takribani fedha za Nigeria Naira bilioni 1 ambazo ni sawa na Dola za Marekani milioni 5.

Magu akizungumza kwenye tukio la kupambana na rushwa katika wizara  ya Serikali  jijini Abuja alisema, “Idadi hiyo itaongezeka kwani  tunataka kufukua wafanyakazi hewa waliojificha ndani kwenye orodha ya malipo ya watumishi wa umma katika majimbo.”

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari  alizindua mapambano  dhidi ya rushwa  serikalini  tangu alipoapishwa Mei 2015. Wizara ya Fedha, Februari mwaka huu ilisema  kuwa iliondoa wafanyakazi hewa wengine 24,000 kutoka kwenye orodha nyingine ya malipo serikalini ambapo kwa mwezi huo iliokoa fedha za Nigeria  Naira bilioni 2.29 sawa na Dola za Marekani milioni 11.5. Magu alibainisha kuenea kwa  udanganyifu unaofanywa kwenye manunuzi ndani ya wizara za Serikali na kwenye huduma za umma na kuonya  watakaokiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Nigeria watakabiliwa na kifungo  cha hadi miaka 10 jela.

Alibainisha kuwa tume imeanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia masuala ya udanganyifu kwenye manunuzi na kikiwa kama wakala wa Serikali kimekuwa kinapokea mashtaka kadhaa kuhusu suala hilo. Alisema tume hiyo imedhamiria kwa kina kuliko ilivyokuwa awali kuondoa shughuli zote za udanganyifu kwenye wizara, idara na mashirika ya umma.

Mapambano dhidi ya rushwa yaliyoanzishwa na Buhari yameshasababisha  kukamatwa kwa watu wenye nafasi za juu serikalini kuhusiana na manunuzi ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.1  kashfa ambayo ilitokea kwa  kununua  silaha katika jitihada za Serikali za kupambana na Boko Haram.

Waliokamatwa kuhusiana na kashfa hiyo ni pamoja na Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa, Sambo Dasuki na Msaidizi wa Rais wa zamani, Goodluck Jonathan, Waripamowei Dudafa, ambaye anatuhumiwa kupokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kutumika kwenye kampeni  za awali za urais kwenye chama cha PDP Desemba 2014.

Licha ya kuanzishwa kwa mapambano hayo dhidi ya rushwa ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Transparency International  ilibainisha kuwa asilimia 75 ya  raia wa Nigeria  wanaamini kwamba rushwa  ndani ya Serikali  ilikuwa imeongezeka katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Ukaguzi uliofanywa kwenye akaunti  za wafanyakazi  kwa kutumia takwimu za kibaiometriki kuthibitisha idadi na kufanya utambuzi wa wamiliki wa akaunti kwenye mabenki ambako hutumiwa na Serikali kulipia mishahara ya wafanyakazi wake, uligundua watumishi wengi waliokuwa wakipokea mishahara  majina yao hayaendani na majina yaliyopo kwenye akaunti na baadhi walikuwa wakipokea  mishahara kutoka vyanzo tofauti.

Hata hivyo Mshauri Maalumu wa Waziri wa Fedha, Festus Akanbi alisema kwamba wizara hiyo imeshafanya ukaguzi wa wafanyakazi 312,000 na kwamba  itakuwa inaendeleza kazi hiyo kwa kutumia mbinu saidizi za ukaguzi kwa kutumia kompyuta katika mapambano yake dhidi ya  rushwa nchini humo.

Rushwa imekuwa ni tatizo kubwa nchini Nigeria tume imeshakamata  Dola za Marekani  trilioni 2 zilizoibwa kutoka kwenye  fedha za umma  tangu kuanzishwa kwake  mwaka 2003

tangu Buhari alipotangaza  mapambano dhidi ya rushwa baadhi ya nakala zinazohusu Bajeti ya mwaka huu zimetoweka  kutoka kwenye Bunge na ukiukwaji mkubwa wa kanuni  kama vile kubainika kwa  Naira milioni 795 sawa na Dola  za Marekani milioni 4 ambazo zimetengwa kwa ajili ya  kuboresha wavuti wa wizara moja kumesababisha  ‘kutumbuliwa jipu’ kwa  Mkuu wa Ofisi ya Bajeti na hivyo kucheleweshwa  kuthibitishwa  kwa mpango wa fedha kwa mwaka 2016.

Katika hili suala la wafanyakazi hewa Tanzania haiwezi kujitofautisha na Nigeria na ni dhihirisho kuwa kila aina ya kadhia ya kifisadi inayofanyika hapa ni sawa na kudurufu kadhia ambayo ilishafanyika huko Afrika Magharibi.

Suala la wafanyakazi hewa limekuwa ni kama kikaango cha watendaji wa Serikali  ya Magufuli kwani wasipolitekeleza kwa makini  huwa inakula kwao, kwani hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela  pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo, Abdul Dachi walitumbuliwa jipu baada ya kudai kuwa mkoani humo hakuna wafanyakazi hewa. Awali ripoti iliyotolewa baada ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa nchini  ilibaini kuwa Serikali imekuwa ikiwalipa wafanyakazi hewa takriban 2,000 kutoka mikoa mbali mbali  na kwamba Serikali imekuwa inapoteza mamilioni ya dola kwa ubadhirifu huo.

Rais wa Tanzania, John Magufuli alitoa siku 15 kwa wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali kufanya ukaguzi na kuwaondoa wafanyakazi hewa serikalini. Rais Magufuli  ambaye  aliingia madarakani  miezi saba  baada ya Buhari  wa Nigeria kuwa madarakani  amejikuta akiwa na changamoto zinazofanana na  zile  anazokabiliana nazo  kiongozi huyo wa Nigeria.

Wafanyakazi hewa waliobainika nchini ambao ni takribani 2,500 wamekuwa wakipokea mshahara  unaokadiriwa kufikia  Dola za Marekani milioni 1.0 kila mwezi.

Hata hivyo baada ya agizo la Rais Magufuli la kusakwa kwa watumishi hao hewa  hivi sasa inakadiriwa kuwa wafanyakazi hao hewa wanakadiriwa kufikia 6,000. nRushwa, ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na vitendo vya ufisadi unaonekana kuwa ni moja ya mambo ambayo alisema  kuwa yamesababisha baadhi ya watu wachache kujiona kuwa wamo peponi huku wengine wakitopea kwenye lindi la ufukara wakiteseka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles